28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 22, 2024

Contact us: [email protected]

TAMISEMI yatangaza Takwimu za uandikishaji wa wapiga kura Uchaguzi serikali za mitaa 2024

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Jumla ya wapiga kura 31,282,331, sawa na asilimia 94.83 ya lengo la uandikishaji, wamejiandikisha kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Takwimu hizi zilitolewa Oktoba 21, 2024, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa alisema kuwa matarajio ya awali yalikuwa ni kuandikisha wapiga kura 32,987,579, lakini zoezi hilo, ambalo lilifanyika kwa siku kumi kuanzia Oktoba 11 hadi Oktoba 20, limefanikiwa kwa asilimia kubwa. “Jumla ya wapiga kura 31,282,331 wamejiandikisha, ambapo wanaume ni 15,236,772 sawa na asilimia 48.71, na wanawake ni 16,045,559 sawa na asilimia 51.29,” alisema Mchengerwa.

Mchengerwa alifafanua kuwa uandikishaji wa mwaka huu umeonyesha ongezeko kubwa la wapiga kura ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, ambapo wapiga kura 19,681,259, sawa na asilimia 86 ya lengo, waliandikishwa. Mwaka huu, serikali imefanikiwa kufikia karibu asilimia 95 ya lengo la uandikishaji.

Aliongeza kuwa uandikishaji huo ulikadiriwa kufanyika kwa asilimia 10 ya lengo kila siku, na matokeo ya siku kumi za uandikishaji yalionyesha mwitikio mzuri wa wananchi. Katika siku ya kwanza, watu 3,882,994 walijiandikisha, sawa na asilimia 11.82 ya lengo la siku hiyo. “Siku ya mwisho, waliandikishwa wapiga kura 4,512,336, sawa na asilimia 13.68 ya lengo la siku, na hii inadhihirisha namna zoezi hili lilivyofanikiwa,” alieleza Mchengerwa.

Aidha, Waziri aliwapongeza wananchi wa mikoa yote 26 kwa kufanya kazi nzuri katika zoezi la uandikishaji, akisisitiza kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yamefanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa haki ya kidemokrasia inatimizwa.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kuwa ni mojawapo ya matukio muhimu ya kidemokrasia kwa Tanzania, ambapo wananchi watapata nafasi ya kuchagua viongozi wa mitaa watakaoongoza kwa kipindi kijacho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles