27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TAMFI wajadili hatua za kuboresha fursa na kukabiliana na changamoto za huduma ndogo za fedha nchini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirikisho la Taasisi zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha Tanzania (TAMFI) limefanya mkutano wa ushawishi ukilenga kujadili na kutathmini mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa. Lengo kuu lilikuwa ni kuboresha ufanisi wa huduma ndogo za fedha na kuhakikisha kuwa taasisi hizi zinaendelea kuwa mhimili wa maendeleo jumuishi ya kifedha nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 4, 2024 wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAMFI, Devotha Minzi, alisema kuwa kikao hicho kililenga kutambua mchango mkubwa wa wanachama wa TAMFI ambao hutoa huduma za mikopo kwa wananchi ambao hawafikiwi na taasisi kubwa za kifedha, ikiwemo mabenki ya kibiashara.

“Ongezeko la mikopo kinachotolewa na wanachama wa TAMFI ni uthibitisho wa uhitaji mkubwa wa huduma za kifedha nchini. Tunawakopesha wateja ambao ni hatarishi zaidi kiuchumi, wale ambao hawana vigezo vya kukopesheka na taasisi kubwa za fedha,” alisema Minzi.

Minzi aliongeza kuwa pamoja na mchango mzuri wa wanachama wengi wa TAMFI, kuna baadhi ya changamoto ambazo zinapaswa kushughulikiwa ili kuimarisha huduma hizo. Alisema, “Malalamiko juu ya gharama kubwa za mikopo, taratibu zisizoridhisha za ukusanyaji wa marejesho, na kukosekana kwa uwazi ni masuala muhimu ambayo tunapaswa kuyajadili na kuyatafutia suluhisho.” Alisisitiza umuhimu wa kikao hicho kwa kutafuta njia za kuboresha huduma ndogo za fedha ili kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Kuhusu mwelekeo wa TAMFI, Minzi alieleza kuwa mkutano huo uliangazia pia Kanuni za Maadili ya Uendeshaji Huduma (Code of Conduct), ambazo zina lengo la kuimarisha uwajibikaji, uwazi, na ushirikiano miongoni mwa wanachama wa TAMFI. Kanuni hizo, ambazo zimegawanywa katika maeneo makuu kumi, zinajumuisha uwazi kwenye gharama za mikopo, utatuzi wa migogoro, na ukusanyaji wa marejesho.

Akizungumzia changamoto na fursa katika sekta hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMFI, Winnie Terry, alisema kuwa huduma ndogo za fedha zinatoa fursa nyingi sokoni ingawa zinakumbwa na changamoto kadhaa.

“Sekta ya huduma ndogo za fedha ina nafasi kubwa ya kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Hata hivyo, tunapaswa kushirikiana na kufuata maadili na kanuni bora ili kuhakikisha kwamba huduma hizi zinakidhi viwango na zinaendeshwa kwa uwazi na ufanisi,” alisema Terry.

Kwa upande wake, Roymez Kway, Muhasibu wa BK Finance Limited, alisema kuwa kushiriki katika mkutano huo kulimsaidia kupata mwongozo mzuri juu ya ushirikiano na taasisi nyingine, na jinsi wanavyoweza kujenga taswira bora kwa wateja wao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka taasisi muhimu za huduma ndogo za fedha nchini kama BRAC Tanzania Finance, SELF Microfinance Fund, na ASA. Pia, wateja waliopata mikopo walitoa ushuhuda kuhusu jinsi mikopo hiyo ilivyoboresha maisha yao, huku wakitoa wito kwa watoa huduma kuendelea kuwa na uwazi na ushirikiano wa karibu na wateja wao.

Mkutano huo ulipokea maoni ya watoa huduma ndogo za fedha na wateja wao, na ulikuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kuboresha sekta hiyo. Wadau wote walikubaliana juu ya umuhimu wa kuimarisha sekta ya huduma ndogo za fedha ili iweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles