TAMASHA la kuinua muziki wa kiasili linalojulikana kwa jina la Marahaba linatarajiwa kufanyika Oktoba 8 mwaka huu, likijumuisha wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Tamasha hilo la muziki wa ‘live’ lilalotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Biafra litaendelea kufanyika bila kiingilio, huku wasanii washiriki wakihimizwa kujitolea ili kuonyesha vipaji vyao kupitia tamasha hilo la kila mwaka.
Bendi ya Marahaba ndiyo itakayokuwa na jukumu la kuwapigia muziki wasanii wengine watakaoburudisha katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanya makubwa siku za usoni, kwa kuwa lengo lake ni kunyanyua muziki wa asili ambao unaonekana kutokubalika sana ndani tofauti na nje ya nchi.
Wakati wa kutambulisha tamasha hilo jana katika ukumbi wa ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza, alionyesha kipaji cha hali ya juu kwa kuimba wimbo wa live kwa lugha ya Kigogo, huku akichanganya na maneno ya Kiswahili.