Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msimu wa Tamthiliya na Filamu za Televisheni za Beijing Afrika umezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam, likiadhimisha miaka 10 ya ushirikiano thabiti kati ya China na Afrika kupitia sekta ya filamu. Tamasha hilo, lililoongozwa na Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, linahimiza urafiki na mawasiliano ya kiutamaduni kati ya mataifa hayo mawili.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi kutoka Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Bodi ya Filamu ya Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na wadau wa filamu kutoka China na Tanzania.
Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Televisheni na Redio ya Beijing, Dong Dianyi, alisema tamasha hilo limekuwa daraja muhimu la mawasiliano ya kiutamaduni.
“Miaka 10 iliyopita, tamasha hili lilianza barani Afrika na sasa ni alama ya urafiki wa kweli kati ya China na Afrika. Tunatarajia kuimarisha ushirikiano huu katika miaka ijayo,” alisema Dong.
Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Bodi ya Filamu ya Tanzania, Emmanuel Ndumukwa, alibainisha mchango wa tamasha hilo katika ukuzaji wa sekta ya filamu nchini Tanzania. Alitaja filamu Karibu Kijijini Milele, iliyotafsiriwa kwa Kiswahili na kushinda tuzo maalum ya kuchangia urafiki kati ya China na Tanzania, kama mfano wa mafanikio hayo.
Ndumukwa aliongeza kuwa tamasha limeleta maudhui mapya, kama Shuke na Beta, filamu ya katuni inayolenga kuvutia watoto wa Afrika. Kwa mara ya kwanza, tamasha limepanua jukwaa lake hadi mtandaoni kupitia programu ya Scooper, ikiwapa watazamaji wa Afrika fursa ya kufurahia utamaduni wa Kichina.
Tangu 2014, tamasha hili limewafikia watu kutoka nchi 13 za Afrika, likionesha filamu 148 katika lugha za Kiswahili, Kiingereza, na Kifaransa. Aidha, limejumuisha matukio ya kiutamaduni kama mashindano ya upigaji sauti, maonyesho ya sanaa ya mapigano, na shughuli za katuni kwa watoto, likionyesha utamaduni wa China kwa njia shirikishi na kuvutia.