KABUL, AFGHANISTAN
KUNDI la Taliban linasema mkataba wake wa amani waliotia saini na Marekani unaelekea kuvunjika.
Kundi hilo linaituhumu Marekani kwa kukiuka mkataba huo kwa kuwashambulia raia kwa ndege zisizo na rubani.
Kundi hilo aidha linadai Marekani inaikosoa vikali Serikali ya Afghanistan kwa kuchelewesha kuachiwa kwa wafungwa 5,000 wa Taliban kama ilivyoafikiwa katika makubaliano hayo.
Taliban ilisema haifanyi mashambulizi dhidi ya vikosi vya Afghanistan na haivishambulii pia vikosi vya kimataifa mambo wanayosema hayakuainishwa wazi kwenye makubaliano hayo ya Februari.
Taarifa hiyo ya Taliban iliyotolewa juzi ilionya kutakuwa na machafuko zaidi endapo Serikali ya Marekani na Afghanistan wataendelea kukiuka makubaliano hayo.
Msemaji wa jeshi la Marekani, Kanali Sonny Leggett lakini alijibu kwa ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa Twitter akisema vikosi vya Marekani vinaendelea kuunga mkono mkataba huo.