KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR
IMEELEZWA kuwa endapo Serikali, wadau na wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji nchini wataungana kwa pamoja katika kupigania haki za watoto, huenda vitendo vya utelekezaji watoto vikaondoka au kupungua kasi yake nchini.
Vitendo hivyo ambavyo wakati mwingine huchangiwa na visa vinavyowakumba kina mama wakati wanapoachana ndani ya jamii, hutajwa kudumaza maendeleo ya watoto.
Akizungumza hivi karibuni mjini Unguja, Ofisa Wanawake na Watoto, Siti Suleiman Juma, alisema asilimia kubwa ya watoto wanaojishughulisha na ajira ni wanaoishi na mzazi mmoja jambo ambalo huathirika kisaikolojia kutokana na kukumbana na kadhia mbalimbali katika jamii.
“Inapotokezea baba kamtaliki mama, basi awashughulikie watoto, unapowadharau watoto na wao watakudharau, kwani itakuwa umechangia kudumaza maendeleo yao, mama pekee hawezi kumudu majukumu yote,” alisema Siti.
Alisema anaona changamoto wakati wanaposhughulikia kesi hizo ni kwa kina baba ambao hawapo kwenye taasisi za Serikali, hawajui wapi pa kuwapata.
Naye Mratibu wa Wanawake na Watoto, Khadija Henoick Maziku, alisema wazazi wakiachana watoto hukumbwa na matatizo mengi ikiwemo kubakwa, ndoa za umri mdogo na mimba, ambayo hurudisha nyuma maendeleo yao.
“Kina baba acheni tabia ya kutoa talaka ovyo na mjione nyinyi ni walezi wa mke na watoto, mwanamke anapokosea mjaribu kusuluhisha sio kumwacha.
“Mwaka jana nilipokea kesi ya mama wa watoto wawili aliyeachwa, alikosa huduma za mtalaka wake tangu ana ujauzito wa mtoto wa pili mpaka amefika miaka mitatu sasa.
“Wote ni watoto wa kiume, wa kwanza amefikia miaka tisa hajapelekwa skuli, linaloumiza zaidi nimegundua ameshaanza kufanyiwa ulawiti.
“Nahadithia kesi ya mama mwingine mwenye watoto tisa, ambao watano hawasomi na wanne wanasoma kwa shida sambamba na kupokea kesi nyingine ya familia yenye watoto wanne ambao wote hawaendi tena skuli,” alisema Khadija.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii, Haroub Suleiman Hemedi, alisema mtoto anategemea nguvu za wazazi wawili, hivyo anapokuwa mmoja pekee huwa hazitoshelezi na huwanyima haki zao za msingi.
Naibu Mrajis Mahakama Kuu Pemba, Abdul-razzak Abdul-Kadir Ali, alisema kesi za baba ambaye hawapatii huduma watoto zipo na hufikishwa katika Mahakama ya Kadhi kwa uamuzi zaidi
“Kuna tatizo, sheria inazungumzia idadi ya pesa kuwa isizidi robo ya mshahara, hivyo kutokana na mshahara ulivyo mdogo hautoshelezi hasa kwa mama mwenye watoto wasiopungua wanne,’’ alisema Abdul-razzak.