Na Walter Mguluchuma- Katavi
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi wamefanikiwa kuokoa na kurejesha Sh milioni 41.117 ikiwamo zaidi ya Sh miloni 23 zilizokuwa zimeibiwa kutoka na kugushi safari hewa na mikutano hewa.
Taarifa ya kuolewa fedha hizo ilitolewa jana na Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa Katavi, Cristophar Nakua alipokuwa akizungumza ofisini kwake jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera.
Alisema Takukuru Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Takukuru Wilaya ya Tanganyika, wameokoa fedha hizo ambazo zilikuwa zimeibiwa.
Alisema Sh milioni 15 ni mali ya Shule ya Msingi Kamjela katika Wilaya ya Tanganyika ambazo zilikuwa zimelipwa kwa mkandarasi Sayi Busines wa Mpanda aliyekuwa akifanya kazi ya kusambaza vifaa vya ujenzi katika Shule ya Msingi Kamjela fedha ambazo zililipwa na kuchukuliwa isivyo halali toka Benki ya NMB Mpanda.
Nakua alieleza kuwa kutokana na kazi aliyofanya mkandarasi huyo alikuwa amelipwa kwa hatua anayostahili lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida Takukuru kupitia Wilaya ya Tanganyika iligundua Sh 15 zilitolewa kinyuma cha utaratibu .
Alisema uchunguzi wa Takukuru ulifanyika na kufanikiwa kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa na waliweza kufanikiwa kuziokoa na kurejesha fedha hizo ambazo zimekabidhiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika, John Romuli ili azirejeshe katika Shule ya Msingi Kamjela.
Alisema fedha nyingine Sh milioni 23 .045 ambazo zilikuwa zimeibiwa na baadhi ya watumishi wa umma kwa kugushi safari hewa na posho hewa za vikao.
Alisema fedha hizo zitaingizwa kwenye mfuko Mkuu wa Serikali kupitia akaunti ya Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ili ziweze kufanya shughuli nyingine za Serikali .
Alisema pia Sh milioni 1.8 zilizokuwa zimekusanywa kama mapato ya Serikali kwa mfumo Point Of Sale (POS) ambazo zilikuwa zimeibiwa na hazikuwasilishwa serikalini kama utaratibu unavyotakiwa zimerudishwa Serikalini ili ziweze kutumika ilivykusudiwa.
Mkuu huyo wa Takukuru alisema Sh milioni 1.7 zilizorejeshwa kutokana na operesheni waliofanya ya kufatilia wadaiwa sugu wa SACCOS ya walimu ya Mpate SACCOS, wamezikabidhi kwa viongozi wa chama hicho ili wawze kuwalipa wanachama wanaoidai.
Kwa upande wake Homera alisema aliwapongeza Takukuru akisema wamekuwa wakifanya kazi zao vizuri na kwa uadilifu kubwa .
Aliwataka wafanye utaratibu wa kuzifanyia ukaguzi SACCOS zote zilizopo katika Mkoa wa Katavi kwani zinachangamoto kubwa ya ubadhirifu wa fedha.
Homera aliwasisitiza wakurungezi wa halmashauri zote za mkoa huo kuwa makini kila wanapokuwa wanaizinisha malipo ili waweze kubaini na mapema ubadilifu wowote ambao unaweza kutokea kwenye halmashauri zao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, John Romuli, alisema Takukuru wamekuwa wakifanya kazi kubwa hivyo wanaiomba kwenye baadhi ya maeneo wanahitaji ushirikiano wa kutoka kwenye Taasisi hiyo .
Alisema asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ambazo zizotolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na wazee zimekuwa hazirudishwi pamoja na jitihada zinazokuwa zinafanywa na halmashauri hivyo wanaomba ushirikiano wa Takukuru kuwasaidia watu wazirejeshe fedha hizo .