AMINA OMARI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, imefanikiwa kuokoa Sh milioni 3.6 ambazo zilitumika kinyume cha utaratibu
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Taasisi hiyo mkoani hapa, Dk. Sharifa Bungala wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu.
Alisema pia walidhibiti Sh milioni 15.3 fedha za umma pamoja na kudhibiti Sh milioni 1.7 zilizotokana na kukamatwa kwa mbao zilizovunwa bila kibali cha serikali.
Alisema taasisi yake, imefanya ufuatiliaji wa miradi 16 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 3.1 ili kujiridhisha kama imezingatia thamani halisi.
“Tumefanya ufuatiliaji wa miradi ya sekta za afya,maji, elimu ,miundombinu ya majengo pamoja na barabara maeneo mbalimbali mkoani humo,”alisema.
Alisema kipindi cha miezi mitatu, wameweza kufanya uchambuzi wa mifumo ili kudhibiti mianya ya rushwa maeneo saba.
“Tumeweza kufanya uchambuzi wa mifumo maeneo saba ambayo ni halimashauri,vyama vya ushirika na uhifadhi wa wanyama pori,”alisema.