Amina Omari, Tanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Tanga inamshikilia Meneja wa Bandari ya Kipumbwi wilayani Pangani mkoani Tanga kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. 900,000.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Anton Gangolo amesema kuwa meneja huyo aliyefahamika kwa jina Steven Mbakweni aliomba rushwa kwa mfanyabiashara ili aweze kumruhusu kusafirisha mzigo toka wilaya ya Pangani kwenda Zanzibar kupitia bandari hiyo
“Uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba Mbakweni aliomba hongo hiyo ikiwa ni baada ya mteja kumpatia nyaraka zinazohitajika zilizotolewa na ofisi ya bandari Pangani baada ya mteja kufanya malipo kwa mujibu wa sheria,” amesema Gangolo.
Aidha ameongeza kuwa nyaraka hizo zilikataliwa na meneja huyo kwa madai kwamba hazitambui na kushawishi apewe hongo ya Sh. 900,000 ili aweze kuruhusu mzigo huo usafirishwe kupitia bandari hiyo.
“Baada ya kupokea taarifa hiyo tuliweza kufanya uchunguzi na kuweka mitego iliyofanikisha kumkamata Mbakweni akipokea rushwa ya Sh. 270,000 ambayo alikubali kupokea Kama hongo baada ya mteja kumbembeleza apunguziwe fedha ambayo awali aliahidiwa kupewa,” amebainisha Kaimu Mkuu huyo.