29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru, mahakama walinde uchumi wa viwanda

Na Ebben Aron, Dar es Salaam

Kwa sasa karibu kila mfuatiliaji wa mambo anajua kwamba ipo dhamira ya kweli ya Serikali ya kuhakikisha taifa hili linaelekea katika uchumi wa viwanda.

Pamoja na mambo mengine, inaonekana kuwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli imejikita kuhakikisha kwamba jambo hilo litakuwa ni mojawapo ya hiba ya utawala wake wakati vitabu vya historia vitakapoandikwa kuhusu utawala wake.

Kama maneno yanayozungumzwa yataendana na vitendo, mipangilio mizuri ya utekelezaji na kwa ushirikiano na wabia wetu wa maendeleo, ndoto hii inaweza kutimia na jamii ya Watanzania kwa ujumla itafaidika. Miongoni mwa viashiria muhimu katika taifa la viwanda ni kuwapo kwa wachapakazi walio na ari wanaoungwa mkono katika kazi zao na Serikali pamoja na sekta binafsi ili wasonge mbele.

Ni jambo la kuvutia kwamba Jumuiya ya Afrima Mashariki (EAC) kupitia mipango yake ya karibuni inaonekana imeanza kuliona hili la ujenzi wa kada ya wachapakazi.

Ni bahati nzuri pia kuwa nchi zote wanachama wa EAC wanaunga mkono mipango hii mipya ya EAC. Kwa upande mwingine, nchi washirika wa maendeleo wa Tanzania waliopo nchini kwa sasa, wameanza kutoa mafunzo ya kitaaluma na kiweledi kwa viwanda vilivyopo nchini ili viweze kuzalisha wajasiariamali watakaoweza kusaidia taifa lao kuvuka kutoka katika umasikini na kwenda pazuri zaidi.

Hata hivyo, ili uchumi wa nchi na wananchi wake wafaidike kutokana na maendeleo hayo, ni muhimu kwa wale wenye dhima ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo, kuweka pembeni masilahi yao na kujali zaidi masilahi mapana ya taifa zima.

Huu ni ujumbe muhimu na ni jambo zuri kwamba hata aliyekuwa Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi, aliutoa wakati wa hotuba yake ya mwisho kama kiongozi wa taasisi hiyo.

Mambo yote na mipango yote inayopangwa kwa ajili ya kuchagiza kile kinachoitwa Tanzania ya Viwanda ni muhimu sana ikaonekana kuwa ina faida kwa wananchi wote na si kwa kundi dogo la wafanyabiashara wenye ukwasi.

Hili ni muhimu kulisema kwa sababu uko nyuma tumeona wafanyabiashara wakubwa na maarufu wakijitapa kwamba wanasaidia kufanikisha Tanzania ya viwanda lakini wanapopata zabuni za Serikali zenye mwelekeo wa kutimiza hilo, wamekuwa wa kwanza kufanya ubabaishaji.

Hakuna shaka kuwa sasa kuna fursa ya kipekee kwa wawekezaji waliopo nchini kufaidika na mwelekeo huu wa Serikali. Bila shaka uhusiano mzuri baina ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu mno katika kufanikisha hilo.

Kinachotakiwa kufanywa kwa nguvu, ari na maarifa yote ni kwa Serikali yenyewe kuwa makini kwa kuweka vigezo vya hali ya juu na ufuatiliaji wa kina kuhusu namna ya kufuatilia na kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo itakayosaidia Tanzania yetu kufika inapotaka.

Katika kutimiza hilo, Serikali haitakiwi kuwa na simile na wafanyabiashara; wawe za kizalendo au wageni, wanaofanya mambo yao kwa viwango vya chini, ubabaishaji na wanaoendekeza rushwa na ubinafsi katika shughuli zao.

Katika vitabu vya historia vitakavyoandikwa kuhusu taifa letu, itaelezwa kwa kina kuhusu namna Serikali zilizopita zilivyoliwa au kutapeliwa na baadhi ya wafanyabiashara waovu waliotumia udhaifu wa ufuatiliaji na kutamalaki kwa rushwa serikalini kujinufaisha wao na kuwaumiza Watanzania.

Nalisema hili pasipo kupepesa macho kuwa kikwazo kikubwa kwa Tanzania kusonga mbele kiuchumi kinatokana na baadhi ya wafanyabiashara waliozoea ubabaishaji na rushwa katika kufanya kazi na Serikali.

Kama tulivyosikia katika vyombo vya habari kuhusu kesi mbalimbali mahakamani na kupitia madai ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wapo baadhi ya wafanyabiashara waliobobea katika vitendo vya kuhujumu jitihada za Serikali.

Ziko namna nyingi ambazo wafanyabiashara hao walizitumia  kuhakikisha wanaihujumu Serikali. Baadhi ya njia hizo ni ukwepaji kulipa kodi, historia mbaya ya nyuma kuhusu kazi walizopewa na utekelezaji mbovu uliotokea na wamesababisha hasara kubwa kuliko inayoonekana vitabuni.

Wapo wafanyabiashara wenye historia iliyotukuka na wako wengine ambao utata umetanda katika shughuli zao.

Ndiyo maana, hatua ya Rais Magufuli kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Diwani Athumani, kwamba apambane na rushwa kwa nguvu zake zote ilikuwa na maana kubwa.

Ni wazi kwamba endapo Takukuru na mahakama zitafanya kazi zake ipasavyo kupambana na rushwa na ubadhirifu, bila shaka hatua kubwa itakuwa imepigwa katika vita hii kubwa.

Tanzania ya viwanda itafanikiwa endapo vita ya rushwa itapiganwa ipasavyo ndani na nje ya Serikali na hili litawezekana kwa kushughulika na makosa ya sasa na nyuma.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles