Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, ambaye anatuhumiwa kujipatia mali nyingi zisizolingana na mshahara wake, amejisalimisha kwa taasisi.
Juzi, Takukuru ilitangaza kutoa donge nono la Sh milioni 10 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa mhasibu huyo baada ya kumsaka bila mafanikio.
Akizungumza jana, Msemaji wa Takukuru, Musa Misalaba alisema mhasibu huyo kajisalimisha na atafikishwa mahakamani wakati wowote.
“Amejisalimisha na muda wowote kuanzia kesho (leo) atafikishwa mahakamani,” alisema Misalaba.
Juzi Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema awali mtumishi huyo alionyesha ushirikiano wa kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili lakini ghafla alitoweka.
Saa chache kabla ya kujisalimisha, Misalaba alikuwa amelidokeza MTANZANIA kwamba kama mtuhumiwa huyo hatajisalimisha ndani ya siku saba, Takukuru ingeomba kibali cha mahakama ili kufilisi mali zote zinazodaiwa kumilikiwa na mtumishi huyo wa umma.
“Tunapenda kuufahamisha umma kwamba tumempa siku saba kuanzia jana Novemba 14 hadi Novemba 20 ajitokeze na asipojitokeza Takukuru itaendelea na taratibu nyingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kuomba amri ya mahakama ya kutaifisha mali zake zote,” alisema Misalaba.
Aidha, katika taarifa ya juzi, Brigedia Jenerali Mbungo alisema nyaraka mbalimbali zilizokusanywa na ushahidi uliopo unathibitisha kwamba mali hizo ni za kwake.
“Ni mali nyingi zenye thamani kubwa, tuligundua kupitia nyaraka mbalimbali ambazo tumezikusanya na ushahidi upo unaothibitisha kwamba mali hizo ni za kwake.
“Kuwa na mali si tatizo, lakini je umezipataje? una maelezo yanayojitosheleza?
“Unaweza kuwa ofisa mdogo lakini una mali ambazo hazilingani na kipato chako lazima maswali yaibuke,” alisema.
Mhasibu huyo anatuhumiwa kujipatia mali nyingi ambazo ni pamoja na maghorofa, nyumba za kawaida za kifahari, magari, pikipiki pamoja na viwanja vilivyo katika mikoa mbalimbali nchini.
Taarifa ya Takukuru inaonyesha mhasibu huyo ana nyumba yenye ghorofa nne iliyoko Ununio Kinondoni, jengo la ghorofa tatu lililoko Kinondoni, nyumba za kupangisha zilizoko Mbweni JKT Kinondoni, jengo la kifahari lililoko Musoma na nyumba nyingine za kifahari zilizoko mkoani Mwanza.
Pia ana viwanja Bunju, Kigamboni, Buyuni (Dar es Salaam), Bagamoyo, Kibaha (Pwani), Kihonda, Kihegea, Lukobe (Morogoro), Kisasa, Itege, Chidachi (Dodoma) na Zuguni, Nyegezi, Nyamuhongolo, Nyamagana, Bagarika (Mwanza).
Viwanja vingine viko Makoko (Musoma), Gomba (Arusha), Mwambani na Mwakidila (Tanga) pamoja na magari matano na pikipiki.