NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema inafuatilia kwa karibu mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliogundulika nchini Uganda na kuchukua hatua mbalimbali kuudhibiti usiingie nchini.
Ili kukabiliana nao, Serikali imenunua na kusambaza mashine maalumu za kupima joto la mwili wa binadamu ikiwa ni hatua mojawapo ya kudhibiti ugonjwa huo.
Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake, Mratibu wa Vituo vya Afya Mipakani wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Remidius Kakulu alisema mashine 12 zimeongezwa na
kusambazwa katika maeneo ya bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA), Kigoma, Songwe, Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga.
“Katika Uwanja wa JNIA na Kigoma awali kulikuwa na mashine lakini kwa kutambua umuhimu wa suala hili tumelazimika kuongeza mashine nyingine ili kuimarisha ukaguzi.
“Mashine hizo pia zimefungwa katika Bandari ya Kigoma, Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa ndege wa Mwanza,” alisisitiza.
Aidha Kakulu aliyataja maeneo mengine ambako mashine hizo zimesambazwa kuwa ni pamoja na Mpaka
wa Mtukula, Horohoro, Kasumulu, Sirari, Murongo, Tunduma, Namanga, Tarakea na Tunduma.
Meneja Kitengo cha Uratibu wa Milipuko ya Magonjwa na Majanga wa Wizara hiyo, Dk. Ali Nyanga alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyegundulika nchini kuwa na ugonjwa huo.