Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema katika Bunge lililopita kuwa Tanzania imepanga kufanya utafiti wa idadi ya samaki katika ziwa Tanganyika kwa kushirikiana na nchi zinazozunguka ziwa hilo zikiwamo DRC, Zambia na Burundi.
Alisema utafiti huo utafanywa na Tasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (Tafiri ) ili kupata picha halisi ya idadi ya samaki na kiwango chake ili kuwezesha kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji kwenye ziwa hilo.
Alisema kukamilika kwa utafiti huo kutatupatia picha halisi ya idadi ya samaki waliopo katika ziwa hilo, hivyo kufanya maamuzi ikiwa turuhusu biashara kubwa ya uvunaji samaki na wizara hivi karibuni itakutana na wadau kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo nchini.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alitaka kujua sababu ya Tanzania kuwazuia wavuvi wa nchini, kufanya uvuvi mkubwa huku wenzao wa Burundi, Zambia na DRC wakifanya hivyo.
Zitto aliitaka serikali kuharakisha utafiti huo na kujua idadi ya wavuvi ili kuruhusu wawekezaji wakubwa kuwekeza katika usindikaji wa samaki.
TAFIRI yataka milioni 300/-
Katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na uwepo wa rasilimali zilizopo katika Ziwa Tanganyika, Taasisi ya Utafi ti wa Uvuvi (TAFIRI) imeomba serikali Sh milioni 300 ili ifanye utafiti katika ziwa hilo, kabla ya kuanza kutafuta wawekezaji, wakiwemo wa viwanda vya kusindika samaki.
Isitoshe ziwa hilo linasimamiwa na Mamlaka ya Ziwa Tanganyika yenye wanachama wan chi hizo tatu ambayo pia inaelezwa inatafuta fedha kwa ajili ya kufanya utafiti kwa ziwa lote.
Utafiti kama huo ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1998, una lengo la kuhakiki idadi ya samaki na aina zilizopo katika ziwa hilo kwa lengo la kuanza kutangaza fursa za uwekezaji wa viwanda vya kusindika samaki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tafiri, Dk Semvua Mzighani aliwahi kuambia vyombo vya habari kuwa kutokana na jitihada za serikali ya awamu ya tano kuhamasisha uwekezaji, wameamua kuomba pesa serikalini ili kufanya utafiti wa rasilimali zilizopo ili kuanza kusaka wawekezaji.
Anasema wameomba fedha serikalini zaidi ya Sh milioni 300 ili kuangalia wingi wa rasilimali za uvuvi, aina ya samaki waliopo na masuala mengine ikiwa ni pamoja na viumbe vingine ziwani.
Alibainisha kuwa utafiti wa mwaka 1998 ulionesha kulikuwa na tani 295,000 za samaki katika ziwa hilo upande wa Tanzania.
Alisema TAFIRI wanatarajia kutumia utafiti kwa teknolojia ya ‘Hydroacoustic’ inayolenga kubaini aina ya samaki kwa kutumia mwangwi unaogonga kubaini kwa pamoja.
Alisema katika utafiti huo, pia wataangalia idadi ya samaki ili kuepuka kuvuliwa kupita kiasi bali kwa kutoa vibali kwa mujibu wa uzalishaji, kwani kwa sasa ziwa Tanganyika halina uvuvi mkubwa kama ilivyo kwa Ziwa Victoria, hivyo baada ya utafiti watawekeza kwa uvunaji mkubwa.
Ziwa Tanganyika
Ziwa lina aina 350 za samaki ikiwamo sangara (Nile perch) wa aina mbalimbali, dagaa, killifish, migebuka, Kapenta na Gibeye na bichir. Ni ziwa refu kuliko yote Duniani na la pili kwa kina nyuma tu ya Ziwa Baikal la Urusi .