27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TADB yajitosheleza kimtaji huku wakulima wakidai zaidi

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam             |              


KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine, amesema  TADB ina mtaji wa kutosha kwa sasa kwa ajili ya kuwahudumia wakulima.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema mtaji wa benki hiyo kwa sasa mahitaji yake yanajitosheleza.

Alisema kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanywa mwaka 2011 wakati wa mchakato wa kuianzisha TADB, ilibainika kwamba mtaji unaohitajika kwa ajili ya kuiwezesha TADB ifikie malengo yake ya kimkakati na kutimiza matarajio ya Serikali na wakulima ifikapo mwaka 2035, ilikuwa Dola za Marekani milioni 500 ambazo zilikuwa sawa na  Sh bilioni 800.

Alisema tangu kuanza shughuli rasmi za ukopeshaji mwaka 2015, Serikali imekuwa ikiendelea kuipatia benki hiyo mtaji.

Kaimu mkurugenzi huyo alisema  mwaka 2015, Serikali iliweka mtaji wa Sh bilioni 60 na mwaka 2017 pia Serikali iliweza kufanikisha kupatikana kwa mkopo wa muda mrefu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo awamu ya kwanza benki ilipatiwa mkopo wa Sh bilioni 104, huku awamu ya pili ikitarajiwa mwanzoni mwa mwaka 2019.

“Kwa hiyo benki ina mtaji wa kutosha kwa ajili ya kukopesha wakulima nchini,” alisema.

Alisema mpaka kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu, Benki ya Kilimo imefanikiwa kutoa mikopo inayofikia kiasi cha zaidi Sh bilioni 48.6 ikiwa ni ukuaji wa Sh bilioni 37.2 katika kipindi cha miezi saba ya mwaka 2018.

“Katika kutimiza maelekezo ya Serikali ndani ya kipindi cha miezi saba ya mwaka 2018, Benki imefanikiwa kukopesha kiasi cha Sh bilioni 37.2 kati ya Sh bilioni 48.6 zilizotumika kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo kupitia mnyororo mzima wa ongezeko la thamani,” alisema.

Justine alisema mikopo hiyo imeweza kuwanufaisha zaidi ya wakulima 520,291, ikiwa na lengo la kuchagiza na kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara nchini.

Wadau wadai fedha zaidi

Gazeti la MTANZANIA lilipoingia mtaani kuulizia ukweli wa mambo, lilitoka na jibu kinzani likidai kuwa mikopo haitolewi  kwa wakulima ambao wamehamasika na hoja ya Serikali ya uchumi wa viwanda ambao unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo ili  kitoe malighafi  kwa viwanda  na vilevile kufanikisha dhana ya kupata ongezeko la thamani kwa mazao yao.

Msimamo huo wa benki unapingwa na wengi wakidai kuwa wakulima wanahitaji mikopo, lakini hawaipati kwa wakati mwafaka na kiasi kinachotakiwa na  isitoshe kuna ukiritimba uliokithiri na unaoingiliwa na masuala ya kisiasa.

Kubwa zaidi lisilopendeza ni  kuwa kigezo kinachotumika na benki hiyo ni neno la kilimo na si shuguli ya kilimo kama kipaumbele na hivyo kuweka mbele wafanyabiashara wa shuguli za kilimo kama pembejeo, ununuzi mazao na udalali wa mazao ambao ni wachache kwa idadi, lakini huchukua kiasi kikubwa  sana  cha fedha badala ya wakulima wenyewe.

“Sisi wakulima tunataka benki ishughulikie mambo yetu kama kupata mikopo ya matrekta, mbolea, madawa na miundombinu ya maghala na mifereji ya umwagiliaji maji; na  mbegu bora za kilimo na si benki kuwapa mkopo wale wanaokuja kutulangua mazao yetu. Hicho si kilimo kwani wanaweza kwenda kwenye benki za biashara wakapata mikopo huko ambako sisi  wakulima hatupati. Ni vizuri TDBA ikaliona hilo na kubakia  kwenye lengo la kuanzishwa kwake na kulifanyia kazi,” anasema mkulima wa miwa wa Morogoro aliyekataa kutajwa jina kwa sababu za wazi  kukataa kubanwa mbavu na benki hiyo.

Mkulima wa Kilosa anasema si sahihi kwa benki hiyo kutosheka na mikopo inayotoa, kwani ni kiduchu sana ukiweka maanani ukubwa wa kundi linaloitwa wakulima ambao ni asilimia 60 ya nguvu kazi nchini ambao wana mchango mkubwa sana kwenye uchumi na Pato la Taifa zaidi ya asilimia 35 na hivyo ingekuwa bora TADB wangefanya juhudi ya kupata mtaji mwingine kutoka umma kwa kuingiza shughuli zao katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).  Alihoji kwanini hawaendi huko ili wigo wa wakopaji  upanuke kwa wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles