Wanafunzi 172 wa Shule ya Msingi Mwinyi katika Manispaa ya Tabora hulazimika kutumia chumba kimoja cha darasa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa shule hiyo, Simon Toyi, shule ina wanafunzi 1721 huku vikiwapo vyumba vya madarasa 10.
Toyi alisema shule ina upungufu wa vyumba 20 vya madarasa kuweza kutosheleza wanafunzi wote ikiwa ni wastani wa kila darasa kuwa na wanafunzi 45.
Alisema shule pia inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo 37 ambako kwa sasa kuna matundu 10 na mahitaji yakiwa 47.
Toyi aliongeza kuwa hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha maendeleo ya elimu shuleni hapo.