Na MURUGWA THOMAS- TABORA
RAIS Dk. John Magufuli amepongezwa kwa hatua anazoendelea kuchukua katika kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na kudhibiti ukwepaji kodi.
Pongezi hizo zimetolewa na viongozi, wadau wa maendeleo na wananchi wa Mkoa wa Tabora waliokutana katika kikao cha kazi mjini hapa.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanry kwa niaba ya wananchi, ambapo alisema uongozi wa Rais Magufuli umeleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, uwajibikaji, kuzuia shughuli zisizo na tija na kuongeza bajeti ya huduma za jamii katika sekta za maji, elimu na afya.
“Rais Magufuli amepongezwa kwa uamuzi wa serikali anayoiongoza kukubali miradi mitano mikubwa kutekelezwa mkoani Tabora ukiwamo wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya Sh bilioni 601 na ule wa upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa ndege.
“Miradi mingine mikubwa ni ujenzi wa barabara zinazounganisha Mkoa wa Tabora na ile ya jirani kwa kiwango cha lami ya Tabora – Nyaua km 85, Tabora – Nzega km 114, Tabora – Pangale km 30, Urambo – Kaliua km 28, Nyaua – Chaya km 85, Tabora – Urambo km 90 na Kaliua – Kazilambwa km 56,”alisema Mwanry.
Tamko hilo pia liligusia miradi mikubwa ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga litakalopita wilaya za Igunga na Nzega pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa.