25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TABIA HATARISHI ZINAZOCHANGIA SARATANI SHINGO YA KIZAZI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WANAWAKE wengi hivi sasa wako shakani kutokana na tishio la saratani ya shingo ya kizazi ambayo ndiyo inaongoza kwa kushambulia kundi hilo.

Takwimu za mwaka 2010 kutoka Shirika la Afya Duniani, (WHO) zinasema kwa Tanzania wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka na 4,355 kati yao hupoteza maisha.

Takwimu za mwaka jana za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), zinaonyesha idadi kubwa ya wagonjwa waliolazwa katika taasisi hiyo ni wanawake na tatizo kubwa linalowakabili ni saratani ya shingo ya kizazi.

Kulingana na takwimu hizo saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inaongoza kwa kushambulia wanawake kwa asilimia 33.

Shingo ya kizazi (Cervix) ni sehemu ya kizazi kati ya uke na mji wa mimba ambayo ina kazi ya kupitisha mbegu za kiume kuelekea katika mji wa uzazi na hatimaye mirija ya uzazi ili kupevusha yai.

Kazi nyingine ya shingo ya kizazi ni kupitisha damu ya hedhi na pia ni mlango anapopitia motto wakati wa kuzaliwa.

Mkuu wa Idara ya Kinga wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, anasema saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya saratani inayoshambulia seli/shembechembe zilizoko ndani ya ngozi laini inayozunguka shingo ya kizazi.

“Tafiti zinaonyesha kwa asilimia kubwa saratani hii ya shingo ya kizazi inasababishwa na kirusi kiitwacho Human papilloma virus (HPV) ambacho huenezwa kwa njia ya kujamiiana.

“Shingo ya kizazi inachukua nafasi kubwa kwa kinamama na kwa hapa Ocean Road ndio saratani inayoongoza kwa wanawake,” anasema Dk. Kahesa.

TABIA HATARISHI

Anasema kuna tabia au hali hatarishi ambazo zinachangia mtu kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Kuanza ngono katika umri mdogo (chini ya miaka 18); “Msichana anayejihusisha na ngono katika umri mdogo ana hatari ya kuweza kupata kirusi cha HPV kutokana na tabia hiyo ya ngono na hivyo anakuwa kwenye hatari kupata saratani hii,” anasema.

Dk. Kahesa anasema tabia nyingine hatarishi ni kujamiiana na mtu mwenye wapenzi wengi, ambapo mwanamume yupo kwenye hatari ya kusambaza kirusi hicho kwa wanawake alionao kwenye mahusiano ya kimapenzi endapo mmoja wa wanawake ana kirusi cha HPV.

Uvutaji wa sigara pia unaweza kumuweka mwanamke kwenye hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Hii ni kutokana na kemikali iliyopo katika moshi wa sigara, mfano wa kemikali hizo ni benzini ambayo inasafirishwa kwa njia ya damu na hivyo inaweza kusababisha saratani sehemu yeyote ile ya mwili ikiwemo shingo ya kizazi.

Tabia zingine hatartishi ni matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula au kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, kutokula mboga za majani na matunda na upungufu wa kinga mwilini.

“Shida ni kwamba hivi vitu havikai kimoja kimoja, unakuta mvuta sigara huyo huyo anafanya uasherati na hatari inaongezeka kunapokuwa na visababishi vingi,” anasema Dk. Kahesa.

DALILI

Dk. Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi huanza na kuendelea kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili zozote.

Hata hivyo anasema kuna dalili ambazo zinaweza kujitokeza wakati ugonjwa upo katika hatua za mwisho ambazo ni pamoja na kutokwa damu isiyo ya hedhi ukeni, kutokwa na damu ukeni baada ya kujamiiana na kutokwa na damu ukeni kwa wanawake waliokwisha kukoma hedhi.

Anazitaja dalili zingine kuwa ni damu inayochanganyikana na majimaji ya uke, matone ya damu au damu kutoka kipindi kisicho cha hedhi, kutokwa na majimaji au uchafu ukeni wenye harufu mbaya na wakati mwingine ukiwa umechanganyika na damu.

Vilevile mtu anaweza kupata maumivu wakati wa kujamiiana, maumivu chini ya tumbo, nyonga na kiunoni, kukojoa mkojo wenye damu, kupitisha mkojo na haja kugbwa kwenye uke na upungufu wa damu.

NAMNA YA KUGUNDUA

“Vipimo vya uchunguzi vinavyofanyika ni pamoja na Pap Smear, kipimo hiki ni rahisi na hakina madhara yoyote. Inashauriwa kufanya kipimo hiki mara moja kwa mwaka,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk. Kahesa, kipimo kingine ni Colposcopy ambacho hutumia darubini kuangalia chembechembe/seli zilizo ndani ya ngozi inayozunguka shingo ya uzazi.

Anasema matibabu ya saratani hutolewa kulingana na hatua ya ugonjwa ambapo ugonjwa ukiwa hatua za mwanzo huweza kutibika kabisa ingawa kuna uwezekano wa kujirudia.

“Hatua za mwanzo za ugonjwa huu huwa haziwezi kupona kabisa, kinachofanyika mara nyingi ni kutoa matibabu yanayotuliza dalili na maumivu na kumuwezesha mgonjwa kuishi vizuri,” anasema.

Anasema huduma za matibabu hutolewa kwa kufanya upasuaji katika hatua za mwanzo za ugonjwa, mionzi, dawa za saratani ama mionzi pamoja na dawa za saratani.

NAMNA YA KUJIKINGA

Anasema mtu anaweza kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi kwa kupata chanjo ya ‘Human Papilloma Visur’, kuepuka ngono katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu, kuepuka kuvuta sigara, kufanyiwa uchunguzi wa saratani hiyo angalau mara moja kwa mwaka, tiba kamilifu ya magonjwa ya ngono (STI) na kupunguza mafuta mengi kwenye chakula.

“Saratani tiba yake ni gharama, mgonjwa anatibiwa muda mrefu na kama kina mama wengi wenye miaka 40 bado wanategemewa waisaidie famila lakini unakuta wanaugua saratani.

“Tusisubiri mtu aumwe, mwelekeo mkubwa iwe ni kwenye kukinga zaidi, tuanze kwa mtu mmoja mmoja, tupeane elimu tujue madhara. Watu wengine wanatumia vitu bila kupima faida na madhara watakayoyapata.

“Kwa saratani zinazotolewa chanjo watu wajitokeze wapate chanjo, na kama wote tukiwazuia tutakuwa tumewaokoa kina mama 1600 hadi 1700 kwa mwaka ambao ni wengi sana. Watu wafanye uchunguzi mapema kuepuka kuona wagonjwa wakiwa katika hatua za mwisho,” anasema Dk. Kahesa.

Hivyo wanawake wanapaswa kuwa makini na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha au kuchochea magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles