26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Taasisi zahamasishwa kuelimisha watoto wenye uhitaji

Na Seif Takaza, Iramba

TAASISI za umma na mashirika binafsi, zimehamasishwa kujenga utamaduni wa kusaidia watoto wanaoishi mazingira magumu, ikiwamo kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kupaza sauti endapo watafanyiwa vitendo viovu.

Wito huo umetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda wakati akizungumza na askari wanawake  katika uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, yatakayofikia  tamati Oktoba 11, 2023 kwenye shule ya msingi Mchanganyiko Kizaga, wilayani humu.

Mwenda amesema watoto wa kike wenye mahitaji maalum,wakielimishwa kwa kina juu ya madhara ya vitendo viovu,watajengewa ujasiri wa kuviepuka kutokana na kuchangia ugonjwa hatari wa UKIMWI na mimba za utotoni.

“Watoto wadogo kwa ujumla ni waoga, hawajui waende wapi kipindi wanapofanyiwa vitendo viovu, elimu kwao ni muhimu mno. Leo tunatengeneza rika hili ili mbele ya safari lije lituongoze, naomba  taasisi zingine ziangalie uwezekano wa kufuata nyayo za shirika la SEMA la mjini Singida”,amesema na kuongeza;

“Shirika hili lilifanya kampeni ya kudhibiti mimba za utotoni na maradhi hatarishi kwa ufanisi mkubwa. Ninayo imani kubwa kwenu kwamba kupitia kauli mbinu yenu ya ‘Ongea nao’,malengo yenu mliojiwekea,mtayafikia,” amefafanua.

Mkuu huyo wa wilaya, ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa kwa uamuzi wa kuwakumbuka watoto hao wenye uhitaji maalum na kuwapatia elimu ya kujikinga na vitendo viovu pamoja na msaada wa vifaa mbalimbali vikiwamo  viatu,kofia,blaketi na dawa za kudhibiti mionzi ya jua.

Kwa upande wake, Kamanda Stella amesema wameona umuhimu kuwatembelea, kuzungumza na kushiriki chakula na wanafunzi wenye uhitaji maalum ili kupata baraka zao.

Stella amesema uzoefu upo wazi kwamba ukimwondolea hofu mtoto mwenye uhitaji maalumu, atakataa kufanyiwa vitendo hivyo na atakuwa na ujasiri wa kutoa taarifa kwa wazazi.  

Katika kuwaelimisha huko, amewataka wanafunzi hao wasikae kimya pindi wanapopapaswa matiti au sehemu za siri,wahakikishe wanatoa taarifa kwa wazazi wao na walimu pia hatua stahiki zichukuliwe mapema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Rose Kibakaya, pamoja na kupongeza Jeshi la Polisi kwa uamuzi wake wa kuwakumbuka wanafunzi wenye uhitaji maalum,amedai kitendo hicho ni tukio la Mungu.

Mwanafunzi mwenye uhitaji maalum, Sawia Nyangu, amemshukuru Kamanda Stella kwa wa kutenga muda kwa ajili ya kutoa elimu kwao juu ya madhara ya vitendo viovu.

Pia Mkuu wa shule hiyo, Haines Kiwelu, ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbali mbali kuwatembelea na kuoana ni jinsi gani wanaweza kuisaidia shule hiyo yenye uhitaji maalumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles