BENJAMIN MASESE-MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ameziagiza taasisi zinazojihusisha na masuala ya bima nchini kujikita zaidi maeneo ya vijijini kutoa elimu badala ya kupigana vikumbo mjini wakigombania wateja ambako wananchi wana uelewa na kipato cha kujitibu muda wowote.
Agizo hilo alilitoa wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya bima yanayofanyika kitaifa mkoani Mwanza katika viwanja vya jengo la biashara la kimataifa la Rocky City Mall ambapo alisema anashangazwa kuona taasisi hizo zikiendelea kupambana katikati ya mji wakati vijijini kuna uhitaji mkubwa.
“Kama tunavyojua sekta ya bima ni sekta nyeti, muhimu na ina mchango kwenye uchumi wa taifa, ninatambua kuwa taasisi hizi zinafanya kazi kubwa kwa ni bima yenyewe ina faida nyingi sana kwa sababu ili biashara na shughuli zote za uzalishaji mali ziwe na uhakika wa usalama kimsingi zinatakiwa kukatiwa bima hivyo niwaombe endeleeni kutoa elimu kwa watu wa makundi yote kwani kuna baadhi yao bado wanamini na wanaichukulia bima kama gharama na kusahau kuwa unapokuwa na bima unakuwa kwenye mikono salama.
“Labda tu niwakumbushe wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla bima ni gharama ila unapokuwa nayo unakuwa na amani muda wote, hata likitokea janga au ajali yeyote kwenye biashara, vyombo vya usafiri na hata kwenye nyumba yako hautahangaika sana.
“Lakini pia kuna changamoto moja taasisi hizi za bima nanyi mmerundikana mjini, ofisi zenu zipo Dar es salaam huku mikoani haumpo, ili muwafikie wananchi wengi zaidi basi mjitahidi kuwekeza nguvu nyingi maeneo ya vijijini, mkifanya hivyo elimu ya bima itaenea nchi nzima na itakuwa na msaada kwa watu wote,” alisema Mongella.
Alisema kama mkuu wa mkoa amekuwa akitembelea vijiji na kuona halisi ya jamii kutokuwa na elimu ya bima na wanapoelezwa wanaonyesha kuwa na uhitaji, hivyo ni wakati muafaka taasisi hizo kutambua asilimia 80 ya watanzania wapo vijijini na kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kufikia asilimia 50 kila mtanzania kuwa na bima ifikapo 2028.