Taasisi za bima zaaswa kuacha kugombania wateja mjini

0
572
Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Yuhoma Education Ltd, Yusuph Yahaya (kushoto) akimwelezea Mkuu Mkoa wa Mwanza, John Mongella majukumu yanayofanywa na taasisi hiyo juzi alipotembelea banda lake wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya siku ya bima yanayofanyika kitaifa mkoani Mwanza.

BENJAMIN MASESE-MWANZA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella  ameziagiza taasisi zinazojihusisha na masuala ya  bima nchini kujikita zaidi maeneo ya vijijini kutoa elimu badala ya kupigana vikumbo  mjini  wakigombania wateja ambako  wananchi wana uelewa na kipato cha kujitibu muda wowote.

Agizo hilo alilitoa wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya bima yanayofanyika kitaifa mkoani Mwanza katika viwanja vya  jengo la biashara la kimataifa la Rocky City Mall ambapo alisema anashangazwa kuona taasisi hizo zikiendelea  kupambana katikati ya mji wakati vijijini kuna uhitaji mkubwa.

“Kama tunavyojua sekta ya bima ni sekta nyeti, muhimu na ina mchango kwenye uchumi wa taifa,  ninatambua kuwa taasisi hizi  zinafanya kazi kubwa  kwa ni  bima yenyewe ina faida nyingi sana kwa sababu ili biashara na shughuli zote za uzalishaji mali ziwe na uhakika wa usalama kimsingi zinatakiwa kukatiwa bima hivyo niwaombe  endeleeni  kutoa elimu kwa watu wa makundi yote kwani kuna baadhi yao  bado wanamini na wanaichukulia bima kama gharama na  kusahau  kuwa unapokuwa na bima unakuwa kwenye mikono salama.

“Labda tu niwakumbushe wananchi wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla bima ni gharama ila unapokuwa nayo  unakuwa na amani muda wote, hata likitokea janga au ajali yeyote kwenye biashara, vyombo vya usafiri na hata kwenye nyumba yako hautahangaika sana.

“Lakini pia kuna changamoto moja taasisi hizi za bima nanyi mmerundikana mjini, ofisi zenu zipo Dar es salaam huku mikoani haumpo, ili muwafikie wananchi wengi zaidi basi mjitahidi kuwekeza nguvu nyingi  maeneo ya vijijini, mkifanya hivyo elimu ya bima itaenea nchi nzima na itakuwa na msaada kwa watu wote,” alisema Mongella.

Alisema kama mkuu wa mkoa amekuwa akitembelea vijiji  na kuona halisi ya jamii kutokuwa na elimu ya bima na wanapoelezwa wanaonyesha kuwa na uhitaji, hivyo  ni wakati muafaka taasisi hizo kutambua asilimia 80 ya watanzania wapo vijijini  na kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kufikia asilimia 50 kila mtanzania kuwa na bima ifikapo 2028.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here