25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

TAARIFA ZA AKAUNTI AIRTEL ZATUA BOT


Na MWANDISHI WETU - Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Idara ya Usimamizi wa Benki wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kened Nyoni, amesema baadhi ya benki zinazomiliki akaunti za fedha za Kampuni ya Airtel Tanzania, zimetii agizo la kuwasilisha taarifa za uendeshaji wa akaunti hizo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu jana pasipo kutaja idadi ya benki hizo, Nyoni, alisema agizo hilo limezingatiwa na kinachofanyika sasa ni kuchambua ili kujua idadi ya benki zisizotii.

Nyoni alisema benki zinazomiliki akaunti za Airtel Tanzania ni nyingi.

“Zipo benki nyingi na baadhi zimezingatia agizo letu tulilolitoa, kwahiyo ni vigumu kukutajia idadi kwa sasa ila jambo la msingi ni kwamba uchambuzi unaendelea ili kubaini benki ambazo hazijawasilisha taarifa tunazozihitaji,” alisema.

Alhamisi wiki hii, BoT iliziagiza benki zilizo na akaunti za fedha zinazomilikiwa na Airtel Tanzania, kuwasilisha taarifa za uendeshaji wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenda kwa taasisi hizo za fedha na kusainiwa na Nyoni, BoT inahitaji kupitia hesabu zote za uendeshaji wa akaunti za fedha zinazohusisha kampuni za simu za Celtel, Zain na Airtel ili iweze kufanya ukaguzi.

Pia taarifa hiyo ilisema BoT ilikuwa inahitaji taarifa za akaunti zote za kampuni hizo kwa mara moja kwa kuanzia Januari mosi, 2000 hadi Desemba 27, mwaka huu (miaka 17) na zinatakiwa kuwasilishwa katika mifumo miwili tofauti ya nakala (hard copy na soft copy) kabla ya saa tano asubuhi ya juzi (Desemba 29, mwaka huu).

Pia katika maelezo yake aliyoyatoa juzi kwa simu wakati akizungumza na gazeti hili, Nyoni, alikiri kwamba wameomba taarifa za akaunti zote za Airtel katika benki na taasisi nyingine za fedha.

Hatua ya BoT kufanya ukaguzi wa hesabu za Airtel, imekuja baada ya hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli, kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kufuatilia kwa karibu umiliki wa Airtel kabla ya mwaka huu kuisha kwa kuwa taarifa alizonazo ni kwamba kampuni hiyo ni mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Pia siku moja baada ya Magufuli kutoa agizo hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kupitia kwa Mwenyekiti wake, Omary Nundu, ilijitokeza na kuitaka Airtel kukabidhi mali za kampuni hiyo kwao kwa kuwa ndio wamiliki halali kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huohuo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema tayari imeshaanza kuwafanyia uchunguzi waliohusika katika sakata zima la uuzwaji wa Airtel kutoka TTCL.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu Alhamisi wiki hii, Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema taasisi hiyo imeishaanza uchunguzi na baadaye wahusika wote watafikishwa mahakamani.

“Tupo tunafuatilia, tumeanza kulifanyia kazi suala hili mara tu baada ya agizo la Rais Magufuli, lakini kwa sasa hatutasema tunawachunguza watu wangapi na wala hatutawataja majina kwa sababu tunahofia kuharibu uchunguzi wetu,” alisema.

Alipoulizwa uchunguzi huo utachukua  muda gani ili uweze kukamilika, alisema  hawawezi kukadiria kwa kuwa suala hilo ni mtambuka na linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

“Suala la uchunguzi ni mtambuka, huwa linategemea zaidi wadau mbalimbali kwa ajili ya kukusanya taarifa, tukisema tutatumia muda gani tutasababisha watu wapate tafsiri mbaya, yupo mtu ambaye anaweza akaona muda uliopangwa mwingi na mwingine akauona mchache,” alisema.

Pia alisema baada ya uchunguzi huo, wahusika watafikishwa katika vyombo vya kisheria ili kujibu tuhuma husika.

Airtel ilisajiliwa Novemba 3, 1998 na uongozi wa TTCL kwa mtaji wa Sh bilioni 200 kwa jina la Celnet na kwa mujibu wa Nundu iliuzwa kijanja na waliokuwa viongozi wa Bodi ya TTCL.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles