JUHUDI zinazofanywa na Serikali ya Marekani na Urusi za kusitisha mapigano ya muda mrefu nchini Syria zinaelekea kukwama baada ya mataifa hayo kushindwa kufikia mwafaka juu ya kufufua makubaliano mapya ya kuendeleza mpango wa pamoja wa kusitisha mapigano ndani ya Syria.
Tayari ushahidi wa mazingira umejipambanua wazi baada ya mmoja wa wajumbe wa Umoja wa Mataifa (UN), Stefan de Mistura, kuzifananisha jitihada hizo na uchungu, ugumu na zenye kukatisha tamaa.
Kundi la kimataifa linaloiunga mkono Syria ikiwemo Marekani, Urusi na mataifa mengine yenye nguvu, lilikutana hivi karibuni katika mkutano wa UN uliofanyika mjini New York kwa ajili ya kuzungumzia ushirikiano mpya wa kusitisha mapigano katika taifa hilo, lakini ghafla Jeshi la Syria likatangaza kuanza mashambulizi mapya ya kijeshi kwa lengo la kuwadhibiti waasi mjini Aleppo.
Inaelezwa kitendo hicho cha Jeshi la Syria kinachangia kiasi kikubwa kuvuruga na kurudisha nyuma juhudi za mataifa hayo kuweka mpango wa pamoja wa kulisaidia taifa hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry kwa upande wake ameweka wazi kwamba amekatishwa tamaa, kwamba ari yake katika mazungumzo imepungua ikilinganishwa na siku za nyuma.
Kerry alisema Marekani na washirika wake ambao wanaunga mkono makundi ya upinzani nchini Syria, wako tayari kurejea katika mazungumzo ikiwa Urusi itaonesha nia thabiti ya kutekeleza makubaliano ya kuweka chini silaha.
Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema upinzani nchini Syria unapaswa kuchukua hatua katika kufikia makubaliano.
Katika hatua nyingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipa timu ya uchunguzi ya kimataifa wiki tano zaidi kukamilisha ripoti yake itakayoeleza nani anayestahili kubeba lawama kufuatia mashambulizi ya gesi ya sumu nchini Syria kitendo ambacho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine yanasisitiza adhabu kali kwa wale waliohusika na kitendo hicho.
Timu hiyo ilipaswa kuwasilisha ripoti yake wiki hii, lakini Katibu Mkuu wa UN, aliyaambia mataifa 15 wanachama katika barua yake ambayo shirika la habari la Reuters limeikariri ikisema kwamba waandaaji wanahitaji muda wa ziada na kutaka icheleweshwe hadi Oktoba 21.
Ripoti ya hivi karibuni kabisa ya baraza la usalama la umoja wa mataifa iliyotolewa mwezi uliopita juu ya uchunguzi wa shirika la umoja huo lenye kudhibiti silaha za kemikali, OPCW inaeleza kuwa Serikali ya Syria ilihusika na mashambulizi mawili ya gesi ya sumu huku Kundi la Dola la Kiislamu lilitumia aina nyingine ya gesi ya sumu.
Wakati hayo yakijiri ndege za kivita zimefanya mashambulizi mazito katika wilaya zinazodhibitiwa na waasi nchini Syria
Hamza al-Khatib ni mkurugenzi wa hosiptali moja katika eneo ambalo linadhibitiwa na waasi upande wa Mashariki mwa mji huo, amekaririwa na DW akisema kuwa watu 45 wameuawa katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia jana.