Na CLARA MATIMO- MWANZA
KAIMU Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, anatarajia kuwaongoza Waislamu wa mkoa huo kuswali swala ya Idd el Hajj itakayofanyika kesho Uwanja wa CCM Kirumba, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake jana, Sheikh Kabeke, alisema lengo la kuwakutanisha Waislamu wote wa mkoa huo ni kudumisha upendo na umoja miongoni mwao.
Alisema wakifanya hivyo itasaidia taifa kuendelea kudumu katika utulivu na wananchi wataishi kwa upendo na kuepuka mifarakano.
“Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) tunaongozwa na kiongozi wetu Mufti Sheikh Abubakar Zubeir, ambaye amekwishatangaza Waislamu wote tutaswali swala ya Idd el Hajj Agosti 12, hivyo lazima tufuate maana Mwenyezi Mungu alisema kila watu lazima wawe na kiongozi wao.
“Kawaida mnapokuwa na kiongozi wajibu wake ni kuwaongoza waliomchagua, hivyo na sisi sikukuu hii tutaswali siku ya Jumatatu.
“Nawaomba Waislamu wenzangu wajitokeze kwa wingi katika Uwanja wa CCM Kirumba siku hiyo ili tushiriki kwa pamoja kusherehekea mahujaji wetu kumaliza hijja yao.
“Waislamu wa Mkoa wa Mwanza tulikuwa tuna muda mrefu sana hatuswali pamoja katika sikukuu za Idd el Fitr na Idd el Hajj, lakini tangu mwaka jana tumeanza kukutana na kuswali pamoja.
“Huu utakuwa ni utaratibu wetu, lakini yote haya yamewezekana kutokana na uongozi thabiti wa mufti wetu Zubeir ambaye tangu aingie madarakani amekuwa na msemo unaotutaka tubadilike, tujitambue na tuache mazoea,” alisema Sheikh Kabeke.
Alisema kuandaa swala si jambo gumu maana hakuna kitu unachobeba mgongoni na kutembea nacho, kinachotakiwa kufanyika ni kukaa na masheikh wa wilaya, mkoa na makatibu kuandaa swala itakayowakutanisha Waislamu pamoja.
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke, baadhi ya misikiti itakuwa wazi siku hiyo ili kutoa nafasi kwa wazee na wagonjwa maeneo mbalimbali, ambao hawataweza kufika uwanjani hapo kuswali.