27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

JPM alilia waliofariki, atoa onyo

Na mwandishi Wetu –Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli, ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao zaidi ya 60 waliofariki dunia kwa kuungua moto walipokuwa wakichota mafuta katika lori lililoanguka eneo la Msamvu mkoani Morogoro jana.

Pia ameonya tabia ya wananchi kuvamia magari yaliyopata ajali kwa lengo la kuchukua bidhaa zilizobebwa.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilisema Rais Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori hilo lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kulipuka moto.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli ameelezea pia kusikitishwa na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbalimbali zilizobebwa na magari hayo na ametaka vitendo hivyo vikome.

 “Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko na kadhalika, nawaomba sana tuache tabia hii,” alisema Rais Magufuli.

Lori hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam lilipinduka majira ya saa 2 asubuhi, jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu baada ya dereva kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.

Taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo na pia amewaombea majeruhi wapone haraka.

“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi, hasa familia za marehemu wote.

“Nawaombea marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka,” taarifa ilimnukuu Rais Magufuli.

Rais pia alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na vifo hivyo.

Pia aliagiza wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa maisha yao.

DK. SHEIN

Rais wa Zanzibar,  Dk. Ali Mohamed Shein, alimtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe kufuatia ajali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma kutoka Ikulu ya Zanzibar, Rais Shein amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa ya ajali hiyo.

“Kwa hakika msiba huu umetugusa wananchi sote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa ghafla na ndugu zetu ambao ni nguvu ya taifa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Vile vile katika salamu hizo za rambirambi, Dk. Shein alimwomba Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema wote na awape nafuu ya haraka majeruhi wa ajali hiyo ili waweze kupata shifaa na waendelee na majukumu yao mbalimbali ya ujenzi wa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles