EVANS MAGEGE
ALIYEKUWA mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Juma Duni Haji ‘Babu Duni’, amesema hamlaumu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Duni, ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti, aliyelazimika kukiacha Chama Cha Wananchi (CUF) na kujiunga Chadema kwa lengo la kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa, ambaye alipitishwa na chama hicho chini ya mwavuli wa vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema Lowassa hastahili kulaumiwa kwa uamuzi huo kwa sababu anajua alichokifanya.
Alitoa kauli hiyo hivi karibuni, katika mahojiano yake na Gazeti la MTANZANIA Jumamosi na kuongeza kuwa CCM wanajua walichokifanya kwa Lowassa hadi yakatokea matokeo hayo.
Duni, ambaye kwa muda mrefu amekuwa pamoja na mkongwe wa siasa upinzani, Maalim Seif Shariff Hamad tangu kuanzishwa kwa CUF, kabla ya katikati ya mwezi huu wote wawili kuhamia chama cha ACT-Wazalendo kutokana na mgogoro wa muda mrefu uliodumu CUF, kwa maneno yake mwenyewe alisema:
“Sitaki kuongea mengi juu ya uamuzi huu wa bwana Lowassa, lakini kwa mtazamo wangu najua hakupenda kuchukua uamuzi huu, ila imembidi tu sababu hakuna namna, huu ulikuwa kama mchezo wa ‘timing’ kakutana na kisu shingoni ikambidi alegeze miguu.
“Lowassa ni mtu mzima, anajua ukweli wake na hata CCM wanajua walichomfanyia. Nyuma ya uamuzi wake tumesikia misukosuko mingi, kuna mashamba, biashara, mara mkwe, lakini sisi si watoto wadogo, tunafahamu yanayoendelea ila ngoja tunyamaze,” alisema Duni, ambaye kwa sasa ni Naibu Kiongozi wa ACT- Wazalendo.
Mwaka 2015 wakati Maalim Seif akitangaza uamuzi wa Duni kuwa mgombea mwenza wa Lowassa, alisema ilikuwa kazi kubwa kumshawishi kukiacha CUF wakati huo na kujiunga Chadema ili awe mgombea mwenza wa Lowassa.
Duni kujiunga Chadema ilikuwa ni mkakati wa vyama vilivyokuwa vikiunda Ukawa kukabiliana na kikwazo cha sheria kupata mgombea mwenza kutoka chama tofauti na ushawishi upande wa Zanzibar.
Akizungumzia kauli ya Lowassa ya kuwataka wafuasi wake waliomuunga mkono kwa kumpigia kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kufikisha idadi ya kura milioni sita kwamba kura hizo wazipeleke kwa Rais Dk. John Magufuli katika uchaguzi ujao, Duni alisema CCM wanajua ukweli wa mambo kwamba hawawezi kufikisha hata hizo kura milioni sita.
Duni, ambaye ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa na ushawishi mkubwa wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alizunguka na Lowassa nchi nzima kuomba kura.
Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Rais Dk. John Magufuli kuibuka mshindi, Babu Duni aliishi ndani ya Chadema kwa miezi takribani mitano tu, kisha akachukua uamuzi wa kurejea CUF.
Akitangaza uamuzi wa kurejea CUF, Babu Duni alikosoa muundo wa uongozi ndani ya Chadema kwa kusema una urasimu mkubwa unaosababisha kila kiongozi katika ngazi fulani kujiona mkubwa na anayeweza kutoa maamuzi yake.
“Ule muundo wake wa kiutawala ni mkubwa mno, bureaucracy ni ndefu sana kiasi kwamba kila mmoja kule ni kambare ana sharubu. Kule kuna (ngazi) Taifa, kuna kanda, kuna mkoa, kuna wilaya, kuna jimbo.
Sasa uamuzi unaweza ukatoka Taifa lakini mtu wa jimbo akasema huo uamuzi mimi siukubali,” alisema Babu Duni.
LOWASSA CCM
Machi Mosi mwaka huu, Lowassa alitangaza kukihama Chadema na kujiunga na CCM.
Alitangaza uamuzi huo katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba, jijini Dar es Salaam, mbele ya Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Magufuli pamoja na viongozi wa juu wa chama hicho.
Katika maelezo yake, alisema amerudi nyumbani na kwamba haoni haja tena ya kuwa mpinzani kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Magufuli, hivyo ameona ajiunge na CCM ili awe sehemu ya kuendeleza gurudumu hilo.
Wiki moja baadaye akiwa mkoani Arusha katika hafla ya kukabidhiwa rasmi kadi ya uanachama wa CCM, aliwaomba Watanzania waliompigia kura katika Uchaguzi Mkuu uliopita kumuunga mkono Rais Magufuli.
“Nimerudi nyumbani, msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani,” alisema Lowassa, huku akiwapungia mkono wafuasi wa CCM ambao walilipuka kwa shangwe na vigelegele.