30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sura ya Tanzania Miaka 17 Bila ya Mwalimu  Nyerere!

mwalimu-nyerereKATIKA moja ya maandiko yake Mwalimu Nyerere alielezea namna ambavyo viongozi wenzake waliomzunguka walikuwa wakinufaika na uwepo wake madarakani. Mwalimu alieleza kuwa kila alipotaka kung’atuka hawa viongozi walio chini yake walikuwa wakimwambia “aah unajua Mwalimu nchi hii bado changa, kwa hiyo bado inakuhitaji usiondoke madarakani”.

Mwalimu katika simulizi yake anasema aliendelea kubakia madarakani mpaka alipogundua kinachoitwa nchi changa ni familia na matumbo ya viongozi waliokuwa wanamzunguka na kumsihi asijiuzulu!

Haya mambo aliyoyasimulia Mwalimu Nyerere leo yanatimiza miaka 32 tangu Mwalimu ang’atuke madarakani na wale viongozi wenzake waliokuwa wakimshauri asijiuzulu baadhi yao tunao mpaka leo na wengi wao ndio hao ambao wamelifikisha Taifa letu ambalo limepitia vipindi kadhaa vya tamu na chungu chini ya uongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Ile sura ya Tanzania ya viongozi wenye uchu wa madaraka, walafi na wabinafsi walioitafuna nchi hii wao na familia zao haikwepeki kuwa  ni mazao ya uongozi Serikali chini ya CCM kwa kuwa hakuna chama kingine kimewahi kushika hatamu ya uongozi wa Taifa hili. Mpaka inapofikia hatua Rais wetu mpendwa kuamua kuunda mahakama ya mafisadi ni ishara tosha kuwa sura ya wezi, walafi, wabinafsi na wahujumu uchumi wa Tanzania waliowahi kuishi enzi za Mwalimu bado wapo na wameendelea kutamba mpaka miaka 32 baada ya Mwalimu kung’atuka na miaka 17 baada ya Mwalimu kutangulia mbele ya haki.

Tangu kuwekwa kwa misingi ya Taifa jipya la Tanzania mwaka 1964,(baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar) hakukuwahi kuwapo mabadiliko makubwa ya kimfumo mpaka sasa. Sina mashaka kuwa wale wale waliokuwa wakinufaika na Mwalimu Nyerere kuwapo madarakani ndio hao hao wanaozuia Taifa hili lisiwe na mabadiliko ya kweli.

Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba kama ingepita ndio yangekuwa mabadiliko makubwa kuwahi kutokea tangu enzi za Mwalimu. Lakini mkwamo wa rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, kutekwa kwa Bunge Maalumu la Katiba na Kushindwa kwa hoja ya Serikali tatu  ni matokeo ya masalia na mabaki ya viongozi walafi, wezi na wabinafsi wanaotaka kuendelea na hulka yao ya kuifaidi na kunufaika na nchi hii wao peke yao na familia zao na vizazi vyao. Hii ndio sura halisi ya Tanzania miaka 17 baada ya Kifo cha Hayati Baba yetu wa Taifa.

Mabadiliko ya mfumo katika rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na hasa uwepo wa hoja ya Serikali tatu ilikuwa ni hatua ya kuzima na kuzitokomeza kabisa sauti za “Mwalimu usijiuzulu unajua nchi hii bado changa”. Uchanga wa nchi hii ambao bado ndio hoja ya watu wanaotaka Serikali mbili ziendelee kuwapo ndio hoja zilizoifikisha nchi hii hapa kiasi cha kuamua kujianzishia wenyewe mahakama ya mafisadi.

Uchanga wa nchi hii ndio uliozalisha kashfa kubwa kubwa kama vile Richmond, ukwapuaji wa fedha za Tegeta Escrow, upotevu wa makontena zaidi ya 2000 bandarini na uchanga wa nchi hii ndio uliomfikisha Waziri Yona na Waziri Mramba gerezani katika kesi ya uhujumu uchumi iliyowakabili. Uchanga wa nchi hii ndio unaomfanya Rais wetu kuendelea kutumbua majipu.

Mfumo tulionao hivi sasa unafanya hii nchi idumae na isikue kwa kuwa sauti za uchanga wa nchi hii hazijaisha. Hakuna namna nyingine ya kubadilisha Taifa hili kama hatutakubaliana kuwa tunahitaji mfumo utakaozika kabisa sauti za uchanga wa Taifa letu. Njia pekee ni kuifufua rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na si kuendelea na hatua ya kura ya maoni kwa rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo staili yake ya kuipitisha imejaa sauti za uchanga wa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles