25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sura mbili za Ibrahim Lipumba ndani ya Cuf na ukawa

Katuni LIPUMBANA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

HATIMAYE Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), huku suala hilo likigubikwa na sura mbili na kauli tata za kiongozi huyo.

Profesa Lipumba amefikia uamuzi huo jana, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kuhitimisha tetesi zilizokuwa zikimuhusisha na kung’atuka katika uongozi wa cha hicho.

Alisema kuwa ameikabidhi Ofisi ya Katibu Mkuu, barua ya kung’atuka nafasi hiyo na anaendelea kuwa mwanachama wa CUF na kadi yake akiwa ameilipia hadi mwaka 2020.

Profesa Lipumba alisema uamuzi wake hakukurupuka bali ameuchukua baada ya Agosti 1, 2015 kutoa taarifa kwa Kamati ya Utendaji ya Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa anatarajia kuwajibika na kujizulu uenyekiti wa Taifa baada ya kukamilisha taratibu za ushirikiano ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ameelezea kuwa kung’atuka kwake kumetokana na kubaini kutoaminika na kuonekana kama kikwazo katika mapambano yanayofanywa na chama chake.

Sababu nyingine amesema ni kusutwa na dhamira yake katika kushindwa kusimamia madhumuni ya kuasisi Ukawa – umoja ambao CUF ni miongoni mwa vyama shirika. Vingine ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi na NLD.

“Nimeshiriki katika vikao vingi vya Ukawa vilivyotufikisha hapa, hata hivyo dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika maamuzi yetu tumeshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa, utu, uzalendo, uadilifu, umoja na uwajibikaji. Rasimu ya Katiba na maudhui yake tumeyaweka kando.

“Walioipinga Rasimu ya Katiba ya Wananchi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba (Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa), ndio tumeamini wataturahisishia kushinda uchaguzi, hivyo tumeshindwa kuongozwa na maadili,” alisema.

Alisema akiwa mwenyekiti wa CUF, alishirikiana ndani ya Ukawa kuelekea katika uchaguzi mkuu kwa nia ya kupata Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi, ikiwamo na kuwa na Serikali yenye kuenzi na kutekeleza yaliyo ndani ya Katiba hiyo yatakayosaidia wananchi kuwajibisha Serikali kutenda haki sawa kwa wote.

Profesa Lipumba, alisema ndani ya Bunge Maalumu la Katiba walianzisha Ukawa kwa lengo la kutetea na kuyaheshimu maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na Tume ya Jaji Warioba na kuwekwa katika Rasimu ya Katiba.

 

BAADA YA KUJIUZULU

Alisema baada ya kujiuzulu, atajikita kufanya shughuli za kitaaluma kwa kujihusisha zaidi na ushauri wa masuala ya uchumi na maendeleo.

“Kujenga uchumi imara unaoongeza ajira kwa vijana, kuhakikisha wajawazito na watoto wanapata lishe bora ili watoto wajenge ubongo na maungo yao wawe na kinga ya mwili,” alisema.

Alisema atajihusisha na usimamiaji wa ujenzi wa miundombinu mizuri kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, nguvu za umeme, mawasiliano na maji na miundombinu inayounganisha nchi jirani.

Profesa Lipumba, alisema atajihusisha na ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali kufikia asilimia 20 ya pato la Taifa na kuhakikisha matumizi ya Serikali yanakuwa na tija.

Aliongeza kuwa baada ya uchaguzi atajikita katika ufanyaji wa utafiti na kutoa ushauri kuhusu maendeleo ya uchumi shirikishi wa Taifa.

 

HISTORIA YAKE CUF

Profesa Lipumba alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa CUF kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Novemba 1999, na akachaguliwa kushika wadhifa huo tena mwaka 2004, 2009 na 2014.

Profesa Lipumba alisema Januari 25, mwaka  2001 katika mapambano yake kwenye chama cha CUF alikamatwa na polisi, kupigwa, kuvunjwa mkono, kuporwa na kuwekwa jela kwa kudai Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, Utawala bora na uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2000 urudiwe.

Januari 27, 2015 alishiriki katika kuandaa na kuongoza maandamano na mkutano wa hadhara kuomboleza mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola Zanzibar, na hasa Pemba Januari 27, 2001.

“Hivi sasa tumebambikiziwa kesi na kushtakiwa kwa kula njama, kufanya vitendo vya uhalifu na kufanya maandamano yasiyo halali, na kesi hiyo ilianza Januari 29, 2015 na bado inaendelea Mahakama ya Kisutu,” alisema.

 

TAHARUKI CUF

Hata hivyo baada ya wanachama kupata taarifa ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba walifurahia na kudai kuwa bora ameondoka katika nafasi hiyo.

Walisema chama ni taasisi na wala si Profesa Lipumba, hivyo basi kuondoka kwake hakuwezi kuathiri chochote shughuli za chama, hivyo basi wanachama waliopo wataendelea kukipigania hadi wanashika dola.

Akizungumzia suala la kujiondoa kwa kiongozi huyo katika ofisi zao zilizopo Buguruni, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Mustafa Wandwi, aliwataka wanachama kutokuwa na wasiwasi juu ya suala hilo kwa sababu Profesa Lipumba amejiuzulu kutokana na matakwa yake.

Alisema wanachama waliowania nafasi mbalimbali ya ubunge na udiwani katika chama hicho wasiwe na wasiwasi, na kwamba wanapaswa kusimama imara ili kuhakikisha wanapata ushindi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

“Chama ni taasisi siyo Profesa Lipumba, hivyo basi kuondoa kwake hakuwezi kuzuia shughuli za chama kutoendelea, wanapaswa kujipanga na kuhakikisha kuwa waliowania nafasi ya uongozi katika kipindi hiki cha uchaguzi wanapata ushindi,” alisema Wandwi.

Alibainisha mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha wanapata ushindi na kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.

 

KAULI YA MWANASHERIA CUF

Akizungumzia kujiuzulu kwa Profesa Lipumba, Mwanasheria wa CUF, Hashim Mziray, alisema katika kipindi hiki ambacho chama hicho hakina viongozi wa juu, kitaendeshwa kwa kufuata katiba ya chama.

Mziray alisema katiba ya chama hicho, Ibara ya 91, inamzungumzia kiongozi wa juu kimamlaka ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho.

Alisema Ibara ya 117 (1) inasema kuwa kiongozi yeyote wa juu wa chama hicho hakiwamo mwenyekiti, anaweza kujiuzulu nafasi yake wakati wowote kwa ridhaa yake mwenyewe.

“Ibara ndogo ya pili inasema ikiwa ameamua kujiuzulu, anapaswa kuandika barua kwa katibu mkuu wa chama ili aweze kuipitia na kuwaambia wanachama wengine juu ya suala hilo.

“Ibara ya 124 inasema kiongozi huyo akishajiuzulu nafasi hiyo, katibu mkuu wa chama anapaswa kuitisha mkutano mkuu baada ya miezi sita ili kujaza nafasi yake. Hivyo basi, tutakapomaliza uchaguzi na kutimiza muda huo, tutaitisha mkutano kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo,” alisema Mziray.

Aliongeza kuwa mkakati wa chama chao ni kuhakikisha kuwa wanaingia kwenye uchaguzi mkuu katika hali ya amani na utulivu, ndipo waanze mchakato wa kutafuta viongozi watakaopeperusha bendera kipindi kijacho.

 

WANACHAMA WANENA

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF, Fatuma Omari Kalembo, alisema kuondoka kwa Profesa Lipumba hakuwapunguzii kitu kwani wataendelea kuunga mkono Ukawa, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani.

“Kwanza Watanzania walimuona (Profesa Lipumba) siku aliposhiriki kumkaribisha Edward Lowassa, sasa leo anapobadilika acha aondoke, sisi tutabaki na CUF yetu na tutaendelea kuunga mkono Ukawa,” alisema Kalembo.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu wa Profesa Lipumba, Abubakari Kitogo, alisema wanampongeza kiongozi huyo kwa uamuzi wake, na kwamba atabeba msalaba kwa kushiriki kumpokea Lowassa kufanya makubaliano ya kuwa mgombea wa Ukawa.

“Tulimuona siku anahojiwa na waandishi wa habari alipoulizwa kuwa wanampokeaje mtu ambaye alikuwa fisadi, lakini alijibu kwa mdomo wake kuwa tangu Lowassa alipojiuzulu, kiwango cha ufisadi CCM kimekuwa kikubwa, sasa leo tunamshangaa.

“Lakini acha aondoke, atabeba msalaba wake na sisi tutaendelea na Ukawa. Watanzania watamhukumu kwa maneno yake kwa sababu CCM ndiyo imetuweka katika matatizo haya yote,” alisema Kitogo.

Naye Kiongozi wa Jumuiya ya Wanawake CUF Ilala, Hafsa Juma, alisema hawajaumia kuondoka kwa Profesa Lipumba kwa sababu kaamua mwenyewe na kwamba watampata mwenyekiti mwingine.

“Ukawa ndiyo tumaini letu, hivyo tutaendelea na mapambano ya kuiondoa CCM madarakani,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na SHABANI MATUTU, ELIZABETH HOMBO NA PATRICIA KIMELEMETA

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles