NA KULWA MZEE,DAR ES SALAAM
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema hali ya maisha nchini imezidi kuwa duni kutokana na kukosekana ushindani sawa wa kisiasa.
Sumaye alisema hayo juzi wakati wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa Ukonga kupitia Chadema, Asiah Msangi.
Alisema kuna ulazima wa kupigania demokrasia ya kweli kwani hakuna mahali kusiko na ushindani maisha yakawa mazuri.
“Lazima tupiganie demokrasia ya kweli, vyama vingine vya siasa viwe na nafasi sawa na CCM ili ushindani uwepo.
“Nilitoka CCM kwa ajili ya Watanzania masikini, tufike mahali vyama vishindane sio vikandamizane,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, alisema matumizi sahihi ya rasilimali ya taifa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
“Tunaweza kuboresha huduma zetu tukapata maendeleo zaidi.
“Ili kuwa na mpango wa taifa wenye vionjo vya Watanzania wote, lazima kuwepo na wabunge kutoka katika vyama mbalimbali bungeni,” alisema.
Kwa upande wake, mgombea Asiah aliwaambia wazee, vijana, wanawake na wazee kwamba hana kanga, vitenge, kahawa na fedha za kuwapa, lakini anaomba wamchague ili awape maendeleo.
“Nitatumia fedha za Mfuko wa Jimbo Sh milioni 70 kuchochea maendeleo, fedha hiyo mkimchagua Asiah Msangi mtaiona,” alisema