31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Sumatra yagoma kushusha nauli

IMG_8336Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema haiwezi kupunguza nauli za usafiri wa mijini kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa kulinganisha na gharama za mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri ni kubwa kwa asilimia 70 wakati gharama na mafuta ni ndogo kwa asilimia 30.
Alisema kabla ya kufikia uamuzi wa kutopunguza bei hiyo, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi ilipitia upya viwango vya nauli kwa kuzingatia mambo saba ikiwamo gharama za mafuta ambazo ni asilimia 30 ya mfumuko wa bei.
“Mambo mengine tuliyozingatia ni pamoja na ushuru wa forodha wa uagizaji wa mabasi mapya, mazingira ya uendeshaji, mabadiliko ya viashiria vya kiuchumi na gharama za utoaji wa huduma za usafiri mijini ambazo ni asilimia 70,” alisema Ngewe.
Alibainisha kutokana na hali hiyo, Sumatra walifanya ukokotoaji wa nauli hizo na kubaini kuwa umbali wa kilometa 0 hadi 10 ni Sh 376.77 ambayo ni sawa na asilimia 5.8 wakati nauli ya sasa ni Sh 400.
Alisema umbali wa kilometa 11 hadi 15 ni Sh 448.62 ambayo ni sawa na asilimia 0.3,wakati nauli ya sasa ni Sh 450 na umbali wa kilometa 16 hadi 20 ni Sh 485.34 ambayo ni sawa na asilimia 2.9 huku nauli ya sasa ni Sh 500.
“Nauli ya umbali wa kilometa 21 hadi 25 ilikuwa Sh 600 ambapo katika ukokotoaji imekuwa Sh 583.34 ambayo ni sawa na asilimia 2.8 wakati nauli ya umbali wa kilometa 26 hadi 30 ilikuwa Sh 750 na katika ukokotoaji Sh 742.74 ambayo ni sawa na asilimia moja,” alisema.
Alifafanua kutokana na hali hiyo, Sumatra imeshindwa kupunguza nauli hiyo kwa madai kuwa punguzo hilo ni dogo na kwamba linaweza kuleta migongano wakati wa malipo na kusababisha usumbufu.
“Tumeshindwa kupunguza nauli kwa sababu gharama zilizopungua ni ndogo na kwamba zinaweza kuleta migogoro kati ya abiria na wahusika wa vyombo vya usafiri,”alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, nauli zilizopo zinapaswa kuendelea kama zilivyo ikiwamo nauli ya mwanafunzi ambayo ni Sh 200, hivyo basi wahusika wa vyombo vya usafiri wanapaswa kuzingatia sheria zilizopo wakati wa kuendesha shughuli zao.
Akizungumzia viwango vya nauli za mabasi ya masafa marefu, Ngewe alisema nauli ya sasa ya mabasi ya daraja la kawaida la chini yanayotumia barabara ya lami ilikuwa Sh 36.89 kwa kilometa ambapo imepungua na kuwa Sh 34.00 ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 7.8.
Alisema nauli ya awali ya mabasi ya daraja la kawaida la chini yanayotumia barabara ya vumbi ni Sh 46.11 ambapo kwa sasa itakuwa Sh 42.50 ambayo ni punguzo la asilimia 7.8 na nauli ya awali ya mabasi ya daraja la kati ni Sh 53.22 kwa hiyo imepungua na kuwa Sh 50.13 kwa kilometa ambayo ni punguzo la asilimia 5.81 na nauli za mabasi ya daraja la kawaida la juu itabaki kuwa Sh 44.96 kwa kilometa.
Ngewe alisema viwango vipya vya nauli vinapaswa kutumika kuanzia Aprili 30 mwaka huu na kwamba Sumatra itawachukulia hatua watakaobainika kutoza kiasi kikubwa cha nauli kuliko kilichotangazwa na mamlaka hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles