Na PATRICIA KIMELEMETA
WAMILIKI wa vyombo vya usafiri hapa nchini wanatarajia kukutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kujadili kanuni za adhabu zinazotarajiwa kuanza Januari, mwakani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mweka Hazina wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi ya Mikoani (Taboa), Issa Nkya, alisema mkutano huo unatarajiwa kufanyika leo na watajadili kupunguza adhabu hizo na kutenganisha makosa ya mmiliki na dereva.
Alisema kanuni hizo zimetungwa makusudi ili kuwakomoa wamiliki wa vyombo vya usafiri, hali inayoweza kusababisha wadau hao kushindwa kutoa huduma hiyo.
“Tunatarajia kufanya kikao na Serikali ambacho kitakuwa na jukumu la kupunguza adhabu na kutenganisha makosa kati ya mmiliki na dereva, jambo linaloweza kupunguza malalamiko,” alisema Nkya.
Alisema sheria hizo zimetungwa na Sumatra na zinaonyesha kuwa, mmiliki anatakiwa kulipa faini ya makosa 57 kwa siku ambayo ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na gharama nyingine za usafirishaji, zikiwamo mafuta na kodi.
Alisema ikiwa Sumatra itaendelea na msimamo wake wa kutopunguza adhabu hizo, watalazimika kufanya mgomo hadi watakapohakikisha suala hilo linashughulikiwa.
“Hatuwezi kulipa zaidi ya shilingi milioni moja kwa siku kutokana na faini za barabarani, wakati magari yanahitaji mafuta na kulipiwa kodi, hivyo basi kama Sumatra inaendelea na msimamo wake, tutalazimika kuweka mabasi yetu nyumbani,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema katika marekebisho hayo, wameiomba Serikali kutenganisha makosa yatakayomhusu mmiliki na dereva, ili kila mmoja aweze kubeba jukumu lake
Alizitaja baadhi ya faini hizo ni pamoja na dereva na kondakta wakivaa sare chafu mmiliki anatakiwa kulipa faini ya Sh 200,000, kuzidisha abiria Sh 250,000, kushindwa kuweka sanduku la huduma ya kwanza Sh 250,000, kuzidisha saa tofauti na muda uliopangwa Sh 250,000.
Alizitaja nyingine kuwa kuzidisha mwendo kasi Sh 250,000, taa ya indiketa ikiharibika Sh 250,000, basi lisilokuwa na ndoo ya uchafu Sh 250,000, wakipiga muziki usio na maadili Sh 250,000, ukikosa ‘reflector’ Sh 100,000, kuweka leseni ya Sumatra sehemu isiyohusika Sh 100,000, dereva kutokuwa na leseni Sh 250,000.
“Kila mwaka mmiliki anatakiwa kuandika ripoti ambayo itawasilishwa Sumatra ili waweze kuangalia utendaji wao na asipofanya hivyo anatakiwa kulipa faini ya shilingi 100,000.
“Itafika kipindi tutashindwa kufanya kazi, kwa sababu faini zilizopo kwa siku ni zaidi ya shilingi milioni moja, hali ambayo inatukatisha tamaa,” alisema Nkya.