28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MRITHI WA MUGABE ATEUWA WANAJESHI BARAZA LA MAWAZIRI

HARARE, ZAIMBABWE

RAIS mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, amewateua maofisa wa jeshi katika baraza lake jipya lenye mawaziri 22 na manaibu 6, ikiwa ni siku tatu baada ya kuvunja baraza la mawaziri, ambalo linaundwa na maofisa wa jeshi waliochangia kumshinikiza Rais Robert Mugabe kuachia ngazi.

Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Misheck Sibanda, alisema mawaziri wote wameteuliwa chini ya kifungu cha sheria cha 104 (1) cha Katiba ya Zimbabwe.

Aliongeza pia, baraza hilo limekuwa dogo kuliko lililotangazwa mwaka 2013 na Rais mstaafu, Robert Mugabe, ambapo kulikuwa na mawaziri 33 na manaibu 26.

Rais Mnangagwa amemteua ofisa mkuu wa jeshi kushikilia wizara muhimu katika serikali yake mpya. Ofisa wa ngazi ya juu katika jeshi aliyetangaza kwenye televisheni ya taifa wiki nne zilizopita kwamba jeshi limechukua udhibiti, Jenerali Sibusiso Moyo, atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Mkuu wa Jeshi la Anga, Perence Shiri, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Kilimo na Maendeleo ya Makazi, Patrick Chinamasa (Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango), Obert Mpofu (Waziri wa Mambo ya Ndani na Utamaduni), Dk. Lazarus Dokora (Waziri wa Elimu ya Msingi na Sekondari), Dk. David Parirenyatwa (Waziri wa Afya na huduma za watoto), Kembo Mohadi (Waziri wa Ulinzi, Usalama na Mavetereani wa Vita), Ziyambi Ziyambi (Waziri wa Sheria na Bunge), Meja Jenerali Sibusiso Moyo (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Kazembe Kazembe (Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni), Mwenyekiti wa Umoja wa Maveterani wa Vita (ZBLWA) Christopher Mutsvangwa ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Huduma za Utangazaji, Dk. Mike Bimha (Waziri wa Viwanda, Biashara na Miradi ya Maendeleo), July Moyo (Waziri wa Serikali za Mitaa na Utumishi wa Umma), Sithembiso Nyoni (Waziri wa Wanawake na Vijana), Profesa Amon Murwira (Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Maendeleo ya Teknolojia), Supa Mandiwanzira (Waziri wa Teknolojia na usalama mtandaoni), Profesa Clever Nyathi (Waziri wa Kazi), Dk. Joram Gumbo (Waziri wa Usafirishaji na Maendeleo ya Miundombinu) na wengineo.

Serikali ya rais huyo mpya haijawashirikisha wanasiasa wa upinzani kama ambavyo ilitarajiwa. Mnangagwa, ambaye aliapishwa Novemba 24, mwaka huu, aliwahutubia wananchi wake, huku akiwataka kudumisha demokrasia.

Mnangagwa alichukua hatamu ya uongozi wa Zimbabwe siku chache baada ya mtangulizi wake, Robert Mugabe, kuachia ngazi kwa shinikizo la jeshi na chama chake kufuatia malumbano ndani ya chama chake cha ZANU-PF kuhusu nani atakayemrithi.

Mugabe alimfuta kazi makamu wake, Mnangagwa kwa kile mkewe  Grace Mugabe alichokitaja kuwa alikuwa na njama za kutaka kumpindua mumewe katika uongozi wa nchi, madai ambayo Mnangagwa alitupilia mbali na kusema ni uongo mtupu.

Kwa mujibu wa gazeti la Guardian la Uingereza, Robert Mugabe ambaye alijiuzulu kwenye uongozi wa nchi ya Zimbabwe akiwa na umri wa miaka 93, atakuwa akilipwa mshahara wa dola 150,000 kila mwezi, huku mkewe, Grace  akilipwa nusu ya hizo, yaani dola 75,000. Mugabe vile vile amekubaliwa kupewa kiinua mgongo cha dola milioni 10,000,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles