RAMADHAN HASSAN -DODOMA
MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) maarufu kwa jina la Sugu, ameliambia Bunge kwamba angekuwa Rais Dk. John Magufuli asingemteua Dk. Mpoki Ulisubisya kuwa balozi, badala yake angemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Akiuliza swali bungeni jana, Mbilinyi alisema kumpeleka Dk. Mpoki nje ya nchi ni kupeleka huduma mbali na Watanzania, kwa vile alifaa kuendelea kutoa mchango wake ndani ya nchi. “Ili kuondoa dhana kwamba wapinzani hawawezi kupongeza, wao kila kitu ni kupinga, leo kwa mara ya kwanza naipongeza Serikali na hasa Dk. Mpoki aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambaye ameteuliwa na Rais (Magufuli) kuwa balozi.
Ingekuwa mimi ningemteua kuwa RC Mbeya, huyu anastahili kuendelea kutoa utaalamu wake,” alisema. Dk. Mpoki aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania, ingawa bado hajapangiwa nchi atakayokwenda kuwakilisha.
Katika swali lake la msingi, Mbilinyi alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha kimeshatolewa hadi sasa kwa ukamilishaji wa ujenzi jengo la kisasa la maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Wizara ya Afya iliomba kutengewa Sh bilioni tano kwa ukamilishaji wa jengo hilo na ununuzi wa vipimo vya kisasa kama CT Scan na MRI Scan.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile alimpongeza mbunge huyo kwa kuipongeza Serikali. Dk. Ndugulile alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilipeleka Sh bilioni moja na baadae katika mwaka wa fedha 2018/2019 wizara iliomba kuidhinishiwa jumla ya Sh bilioni tano kwa ukamilishaji mradi wa ujenzi wa jengo la huduma za radiolojia na jengo la wazazi Meta katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya.
Naibu waziri huyo alilieleza Bunge kuwa hadi sasa kiasi cha Sh bilioni tatu zimeshapokewa kwa kazi hizo, ambazo Sh bilioni mbili ni kwa kumalizia mradi wa ujenzi wa jengo la radiolojia na ununuzi wa baadhi ya vifaa vyake. Alisema Sh bilioni moja ni kwa kugharamia ujenzi wa jengo la wazazi Hospitali ya Rufaa Meta.
“Tayari ujenzi huo umeshakamilika kwa asilimia 90 na kwa sasa mafundi wanakamilisha kuingiza umeme katika jengo baada ya ununuzi wa transfoma,” alisema. Hivyo hadi kufikia mwezi Machi 2019 litakuwa limekamilika rasmi.
Alisema Serikali tayari imeshanunua CT Scan kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo inasubiria kukamilika kwa jengo maalumu ili iweze kusimikwa rasmi na vile vile hospitali inategemea kupatiwa mashine ya MRI kupitia mradi wa ORIO wa Wizara ya Afya.