Waziri wa Ulinzi aliyeapishwa Alhamisi kuwa rais wa baraza la mpito la kijeshi Ahmed Awadh Auf amejiuzulu wadhifa huo na nafasi yake kuchukuliwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan Abdulrahman.
Awadh Auf ametangaza hatua hiyo siku moja baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais al-Bashir na yeye kushika hatamu.
Kwenye hotuba yake ya kujiuzulu, iliyorushwa kwenye televisheni Awadh Auf alisema anaachia wadhifa huo kwa maslahi ya taifa na kwa kuwa taifa hilo lina watu wazuri na jeshi la kuaminika. Amesema ana imani kwamba makundi hayo mawili yatafanya kazi pamoja.
Jeshi liliwahakikishia raia kwamba halina mpango wa kuongoza kwa muda mrefu. Baraza hilo pia lilisema utawala wa kijeshi wa miaka miwili ya mpito unaweza kubadilishwa na kuahidi kwamba linaweza kuvunjwa muda mfupi ujao iwapo kutafikiwa suluhu ya mzozo wa kisiasa unaolikabilia taifa hilo.
Raia walionekana kufurahishwa na hatua hiyo ya ghafla ingawa jeshi liliwahakikishia kwamba halina nia ya kutawala moja kwa moja.
Awadh Auf alikula kiapo cha kuongoza baraza hilo la mpito usiku wa Alhamisi muda mfupi tu baada ya rais al- Bashir kupinduliwa na kukamatwa.
Kuondolewa kwa Bashir kulifuatia miezi kadhaa ya maandamano yaliyokuwa yakiipinga serikali, lakini hata hivyo waandamanaji walisema hawakufurahishwa kuona nafasi yake inachukuliwa na waziri wa ulinzi ambaye ni sehemu ya serikali yake iliyodumu kwa muda mrefu.
Kundi linaloratibu maandamano limesema kwamba kujiuzulu kwa Auf ni ushindi kwa matakwa ya raia na kuahidi kwamba waandamanaji wataendelea kusalia mitaani hadi kutakapopatikana serikali ya kiraia.