25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Spika amtaka CAG ajiuzulu

*Asema anampa wakati mgumu Rais Magufuli

*Aikubali ripoti yake ya ukaguzi

NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kujiuzulu kwani anampa wakati mgumu Rais Dk. John Magufuli.

Akisisitiza hoja yake, Ndugai alisema hana chuki binafsi na Profesa Assad na ni rafiki yake lakini ugomvi wao uko katika matamshi kwa kile alichodai kuwa anatumia lugha za udhalilishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema kitendo cha Profesa Assad kuendelea kutumia neno dhaifu ni kielelezo kuwa hiyo ni dharau na kejeli kwa mhimili huo muhimu.

“Tatizo letu ni maneno ambayo Profesa Assad aliyasema Marekani na juzi alipoita waandishi alisisitiza ataendelea kuyatumia, hilo ndilo tatizo sisi tuliyakataa.

“Matusi anayoyatoa kwa kujua ama kwa kutokujua narudia tena namwambia rafiki yangu Profesa Assad hili jambo aliache, anampa mheshimiwa rais wakati mgumu,” alisema Ndugai.

Alisema wanafanya kazi vizuri kwa upande wa taarifa lakini tatizo ni Profesa Assad ambaye amekuwa akitamka maneno aliyodai kuwa si mazuri.

“Profesa Assad hakupaswa na wala hapaswi kulitukana Bunge kwa lugha za rejareja, alihojiwa na kamati akasimamia msimamo wake na Bunge likapitisha azimio, amefanya kosa linaloitwa ‘contempt of Parliament’ kwa kuendelea kutumia maneno tuliyoyakataa.

“Anapaswa kuona busara ni ipi katika haya kwa sababu hana mtu wa kufanya naye kazi zaidi ya Bunge,” alisema Ndugai.

Alisema Bunge huendesha mambo yake kufuatana na taratibu za bunge na kumtaka Profesa Assad aeleze alipata wapi mamlaka ya kufanya kazi ambayo si yake.

“Ni neno ambalo ‘auditor’ analitumia anapofanya ‘entity’ na akishamaliza kazi yake anataarifu ‘stakeholders’, kwa upande wa Serikali ‘shareholder’ ni Bunge kwa niaba ya wananchi, anachosema Serikali ndio ‘weak’ katika udhibiti wa fedha.

“Badala ya kuelekeza anatumia kundi ambalo halihusiki, tunasimamia mambo mengi yeye amewekwa na Serikali kama jicho kuangalia na kutuambia sisi hawezi tena kugeuka akafanya alichofanya,” alisema.

Spika Ndugai alisema neno hilo halina heshima kwa mhimili wa Bunge kwa sababu wao wanafanya kazi nyingi kwa niaba ya Watanzania.

“Tulipomuita kwenye kamati aliambiwa atoe kamusi ya kihasibu yenye neno hilo wala hakuwa nayo, ni neno ambalo hatulipendi na kama mtu mstarabu ukiambiwa mtu hataki acha…kama unalipenda sana basi jiite mwenyewe.

“Na kuonyesha hatulipendi tumechukua hatua kali sana kwa Mdee (Mbunge wa Kawe) na Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) wale ni wabunge wenzetu hatunachuki nao lakini tumechukua hatua.

“Tunasisitiza hatupendi unasema utaendelea kulitumia…nitakuita tena, nadhani itakuwa mbaya zaidi, hatuwezi kujenga nchi kwa namna hii. Shida mtu akishasoma anaona watu wengine mbuzi tu, lazima tukemee mambo haya, tuwarudishe wasomi wetu warejee kwenye mstari,” alisema.

Alisisitiza kuwa Bunge lilishatoa azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad na kwamba huo ni uamuzi halali na hauingiliwi na mtu yeyote.

“Wananchi wanaona hawa ni watu wetu wewe unaona dhaifu, lazima tukatae si sehemu ya utamaduni wetu na tusingependa kama nchi yatufikishe yalipotufikisha,” alisema.

TAARIFA YA CAG

Alisema Rais aliwasilisha ripoti hiyo bungeni kupitia wasaidizi wake na kwa sasa ni mali ya Bunge hivyo wataifanyia kazi hatua kwa hatua.

“Hakuna tatizo katika suala la ripoti ni ripoti za kawaida kama zilivyo zingine, nikifika Dodoma nitaagiza taarifa zipelekwe katika Kamati za LAAC na PAC.

“Kilichowekwa mezani ni ‘audit querries’ si ukweli wenyewe kwamba kila aliyetajwa mle ni mwizi. Kazi ya kamati ni kuwaita wahusika na kuwasikiliza watoe ufafanuzi kama kulikuwa na vocha hazikuonekana.

“Tukijenga utamaduni kwamba mtu akitajwa tu basi amehusika moja kwa moja tutakuwa hatuendi sawa,” alisema Ndugai.

Spika alisema wataifanyia kazi ripoti hiyo na Watanzania watapata mrejesho wa kila jambo lililotajwa kwenye ripoti lakini akasisitiza kuwa msimamo wao wa kutofanya kazi na Profesa Assad uko palepale.

“Bunge halifanyi kazi na Profesa Assad ni uamuzi ‘serious’ wala si wa kujoki hata kidogo, tutaendelea kufanya kazi na ofisi ya CAG ina wakaguzi wengi mfano ikitokea akifa leo Profesa Assad kwani ofisi itakuwa imekufa au leo Ndugai akifa Bunge halitaendelea?,” alihoji Ndugai.

 MATIBABU YAKE

Spika Ndugai alisema suala la gharama za matibabu yake halihusiani na mgogoro huo na kwamba hata hospitali aliyokuwa akitibiwa ni ya kawaida.

“Nilikaa kwenye matibabu kwa muda mrefu 2015/2016, binadamu tunaugua na matibabu hupangi wewe hivyo, kama kuugua kwangu kuliligharimu taifa fedha nyingi mimi sijui…labda ningekufa.

“Hospitali niliyoenda kutibiwa ni ya kawaida na nilikuwa nakutana na Watanzania wenzangu kila siku, yeyote anayekwenda kutibiwa India anakwenda kwa utaratibu wa Serikali sasa inategemea anayeumwa kidonda au moyo.

“Na wanaotibiwa sehemu tofauti ni wengi sasa mimi nifanyeje kama mtu akiamua kwenda kutibiwa kokote?” alihoji Ndugai.

KIINI CHA MGOGORO

Mgogoro baina ya Profesa Assad na Bunge ulianza baada ya kiongozi huyo kusema kuwa Bunge ni dhaifu kwa kile alichodai kuwa limeshindwa kuisimamia Serikali.

Profesa Assad alitoa kauli hiyo Desemba mwaka jana alipokuwa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York ambapo alisema Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo Serikali.

Kauli hiyo ilizua mjadala na Spika Job Ndugai alilieleza Bunge kuwa Profesa Assad alionesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.

Januari 21 Profesa Assad alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilimtia hatiani kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka, alisema wamejiridhisha kuwa Profesa Assad alilidhalilisha Bunge kwani alikiri mbele ya kamati kuliita Bunge dhaifu lakini alipingana na tafsiri ya neno ‘dhaifu’ iliyopo kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu inayosema ‘goigoi, hafifu, isiyo imara’ akisitiza kiuhasibu udhaifu ni ‘upungufu’.

Kamati hiyo pia ilimtia hatiani Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), ambaye aliunga mkono kauli hiyo ya CAG na kupendekeza asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia Aprili 2.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles