Loveness Benard – Bunjumbura
TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imelazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Burundi, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022 nchini Qatar.
Matokeo hayo yana maana kwamba, sare au ushindi wa aina yoyote katika mchezo wa marudiano utaivusha Stars hatua inayofuata.
Mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na Burundi utapigwa Septemba 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa jiji Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana, wenyeji ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza dakika ya 80 kupitia kwa Cedric Hamis lakini Taifa Stars ikafanikiwa kusawazisha dakika ya 85 kupitia kwa Simon Msuva.
Msuva alifunga bao hilo baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Burundi pamoja na kipa wao Jonathan Nahimana.
Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi langoni mwa Burundi dakika ya 14, ambapo mkwaju wa Mbwana Samatta uliokolewa na Nahimana.
Burundi ilijibu shambulizi dakika ya 16, ambapo kipa wa Taifa Stars, Juma Kaseja aliokoa mchomo wa hatari.
Taifa Stars itajutia makosa iliyofanya dakika ya 12, baada ya Msuva kukosa bao akiwa amebaki yeye na Nahimana, kwani mkwaju wake ulipanguliwa kabla ya mpira kumfikia Samatta ambaye shuti lake lilitoka nje.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu kila moja ikisaka bao la kuongoza.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa kwa milango ya kila upande kugoma kufunguka.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, dakika ya
48, beki wa Taifa Stars, Erasto Nyoni almanusura afunge bao lakini baada ya mkwaju wake wa kiufundi kutoka nje kidogo ya lango la Burundi.
Dakika ya 58, Samatta aliwachambua mabeki wa Burundi na kuingia eneo hatari lakini alikosa utulivu baada ya shuti lake kutoka nje.
Taifa Stars ilindelea kuliandama lango la Burundi, dakika
ya 68 Iddy Seleman alikosa maarifa ya kuutumbukiza mpira kwenye lango la
Burundi, baada ya kupiga shuti
dhaifu.
Dakika ya 80, Cedric Amissi aliwainua mashabiki wa Burundi baada ya kufunga bao kwa shuti lililomshinda Kaseja.
Taifa Stars ilijibu mapigo dakika ya 85 na kufanikiwa kusawazisha kupitia kwa Msuva.
Dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
tunapojitaidi tujipongeze dalili ni nzuri,taifa star ongezeni kujiamini!kila la heri