29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi waaswa kujikinga maambukizi ya VVU

Khamis Sharif -Zanzibar

WAFANYAKAZI na wadau wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), wameaswa kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na kutohadaika na uwapo wa takwimu ndogo ya watu wanaoishi na VVU visiwani Zanzibar.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa ZIC, Abullnassir Ahmed, wakati akifungua mafunzo ya kuangalia namna ya kujilinda na maambukzi ya VVU kwa wafanyakazi na wadau wa shirika hilo.

Alisema kutokana na juhudi zilizofanywa na Serikali kupitia Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), hali ya maambukizi imeripotiwa kushuka hadi kufikia asilimia 0.4, na bado kuna watu wanaendelea kutochukua hatua.

Ahmed alisema hali hiyo ilitokana na watu waliofika vituo maalumu kuchunguza afya zao na baada ya kugundulika kuamua kujitangaza.

“Nyinyi wadau endeleeni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuzuia maambukizi mapya, tunasikia idadi ya wagonjwa imepungua kwetu, tusibweteke,” alisema.

Akiwasilisha mada ya hali ya Ukimwi katika mafunzo hayo, muwezeshaji kutoka ZAC, Sihaba Saadat, alisema hali ya maambukizi kuanzia mwaka 2007 hadi 2017 imeonyesha kushuka Zanzibar na kufikia 0.70 kutoka asilimia 0.83 mwaka 2007.

Alisema mwaka 2017, wananchi 159,771  Zanzibar walichunguza afya zao, ambapo kwa Unguja waliochunguza walikuwa 130,466 na 1,326 waligundulika kuishi na VVU sawa na asilimia 1.0, wakati kisiwani Pemba waliochunguza walikuwa 29,245 na kati ya hao 66 waligundulika na wameathirika sawa na asilimia 0.6.

Alisema kwa upande wa Unguja, wilaya inayoongoza ni Wilaya ya Kati, ambayo wananchi wake 10,779 walichunguzwa na 159 sawa na asilimia 1.5 waligundulika kuwa na VVU.

Kwa upande wa Pemba, Wilaya ya Micheweni iligundulika na idadi ya wananchi 33, sawa na asilimia 0.7, iliyotokana na wananchi 5,009 waliochunguzwa, ikifuatiwa na Wilaya ya Chakechake ambako waligundua wananchi 55, ingawa 9,920 ndio waliochunguza afya zao, sawa na asilimia 0.6.

Alisema mwaka 2007, walipofanya utafiti kwa wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsi moja, ilikuwa ni asilimia 12.3, wakati mwaka 2012 ilishuka hadi kufikia asimilia 2.6.

Akizungumzia kuhusu kundi la wanawake wanaokodisha miili yao (madada poa) kwa mwaka 2007, hali ya maambukizi ilikuwa asilimia 10.8, wakati mwaka 2012 walipowachunguuza tena ilipanda na kufikia 19.3.

Kwa kundi la vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, hali ya maambukizi ilikuwa kubwa mwaka 2007 kwa kufikia asilimia 16, ambapo mwaka 2012 iliripotiwa kupungua hadi kufikia asilimia 11.3.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, walisema ufahamu upo wa mambo yanayohusiana na VVU, ingawa ni vyema juhudi zikaendelezwa kufanywa.

Aisha Abdalla Rashid kutoka Idara ya Mazingira, alisema wapo wanaopata VVU kwa kubakwa, hivyo ni vyema mahakama na wasimamizi wengine kutoa adhabu kali kwa wabakaji.    

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles