COLOMBO, SRI LANKA
RAIA wa Sri Lanka wameandamana kumshinikiza Rais Maithripala Sirisena kuitisha kikao cha Bunge mara moja ili kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa hapa.
Zaidi ya watu 10,000 wakiwemo wabunge na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wameandamana mjini hapa, wakiimba nyimbo mbalimbali wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema; “Tuushinde udikteta unaoidhoofisha katiba, turejeshe demokrasia, zingatia katiba na Bunge lirejelee vikao ili tusitishe mgogoro.”
Baadaye walifanya mkutano karibu na nyumba ya waziri mkuu.
Maandamano hayo yanajiri siku moja baada ya Spika wa Bunge, Karu Jayasuriya kuonya kuwa huenda kukashuhudiwa ghasia iwapo wabunge hawatarejea bungeni mara moja.
Rais Sirisena alimfuta kazi Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe na baraza lake la mawaziri Ijumaa wiki iliyopita na kumteua Mahinda Rajapaksa kuchukua wadhifa huo.
Wickremesinghe anataka vikao vya Bunge virejeshwe akisema ana uungwaji mkono wa idadi kubwa ya wabunge.
Jumamosi iliyopita, Rais Sirisena alisitisha vikao vya Bunge ikiwa ni njia mojawapo ya kumpa Rajapaksa muda wa kupata uungaji mkono wa kutosha ili asikabiliwe na kura ya kutokuwa na imani naye.
Hatua ya Rais Sirisena kumfuta kazi Wickremesinghe imetajwa na baadhi ya waangalizi kuwa ingezua migogoro ya kikatiba.
Siku ya Jumapili, watu wawili waliuawa na mwingine kujeruhiwa baada ya ufyatulianaji risasi katika ofisi ya Wizara ya Mafuta, tukio ambalo linadaiwa kusababishwa na mgogoro huo.
Marekani imesema inafuatilia matukio nchini Sri Lanka huku ikimtaka Rais Sirisena kuitisha vikao vya Bunge.
Rais huyo alisema amemfuta kazi Wickremesinghe kutokana na madai ya kuhusika kwa waziri mmoja katika mpango wa kutaka kumuua.
Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo na Wickremesinghe amekanusha madai hayo.