Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Spika wa Bunge, Job Ndugai ameliomba Bunge limsamehe na kumpuuza Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Afrika (PAP) na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele ambaye anatuhumiwa kwa kutokuwa na nidhamu kwa kuichonganisha Serikali na Bunge.
Spika Ndugai aliitaka Kamati ya Haki, Madaraka na Maadili Jumatatu, Mei 20, kumhoji Mbunge huyo na leo Mei 23, kamati hiyo imetoa taarifa ya kumsamehe mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
“Bunge katika uendeshwaji wake ni lazima tuangalie vikao vingine vya bunge vilivyopita, mambo yaliyotokea na kwa muda mrefu hakukuwahi kutokea mambo kama haya.
“Mheshimiwa Samweli Sitta, katika mazingira kama haya aliwahi kuliomba bunge kumpuuza mbunge fulani, kwa maana hiyo nami nawaomba tumpuuze Masele na tumsamehe, tuendelee na mambo ya maana, hatuna ubaya na mtu yeyote,” amesema Ndugai.
Aidha Spika huyo amewataka wabunge kuacha kupeleka maneno ya umbea kwa Rais Dk John Magufuli kwa kuwa maneno hayo yanamyumbisha na kumchanganya Rais katika utendaji wa kazi zake.
“Muoneeni huruna mheshimiwa rais, anafanya kazi kubwa sana acheni kupeleka umbea, uwongo na fitina kwa rais tunamyumbisha, tunamchanganya na kumzeesha acheni kuwagombanisha Waziri MKuu na Spika migongano ya nini, nilipeleka hiki kwa viongozi wangu, nilipeleka hivi, uchonganishi mtupu hamna ukweli wowote.
“Tuache hiyo tabia, unajambo njoo kwa spika wewe ni mbunge unaweza kuchukua wabunge wenzio wenye heshima zao mje kwa Spika, sema jamani mimi Spika hanitendei mema tutaelewana tuu acheni ushabiki wakupiga piga makofi,” amesema Spika.