26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SPIKA, CHADEMA VITANI

WAANDISHI WETU, DODOMA NA DAR ES SALAAM

VITA ya maneno imeibuka kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Chanzo cha vita hiyo mpya ni matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) uliofanyika Aprili 4, mwaka huu, baada ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwapigia kura za hapana wagombea wa Chadema, ambao ni Lawrence Masha na Ezekia Wenje.

Pia vita hiyo ikachochewa na tukio la juzi la Ndugai kuagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge, baada ya kudaiwa kumtukana na kauli yake aliyoitoa bungeni juzi ya kukitaka chama hicho kizingatie mikoa katika kuwasilisha upya majina ya wagombea wa nafasi mbili za EALA.

Baada ya Ndugai kutoa kauli hiyo, chama hicho kupitia taarifa ya Mkurugenzi wake wa Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, kiliipinga vikali kwa kusema hatua hiyo ni sawa na kutengeneza vigezo vingine nje ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Sheria yake ya Uchaguzi na Kanuni za Bunge.

Kupitia taarifa hiyo, iliyosambazwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Mrema alisema wanalaani na kupinga kauli za Ndugai kwa sababu zinapotosha, zinaudhi na zina lengo la kuligawa Taifa katika misingi ya udini, ukabila na jinsia.

“Tunapinga kwa nguvu zote kitendo hiki na vingine vya namna hiyo, vinavyolenga kutaka kuligawa Taifa letu na tunawataka Watanzania wenye nia njema na nchi yetu kutafakari madhara ya kauli za Ndugai na kuzikemea kwa nguvu zote,” alisema.

Mrema alisema lengo la chama hicho, kilichowahi kususia vikao vya Bunge hilo vilivyokuwa vikiongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wawakilishi ndani ya EALA wenye weledi na uwezo wa kujenga hoja na kusimamia maslahi ya nchi yetu.

“Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya uwakilishi kutoka Tanzania uliochangiwa na maspika waliopita kwa kutozingatia matakwa ya ibara ya 50 ya Mkataba wa EAC na masharti ya Kanuni ya 12 na nyongeza ya tatu ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, mwaka huu. Hii ilifanya nchi kuwa na uwakilishi hafifu kwa sababu ya ushabiki wa kisiasa,” alisema.

Pia alisema wanamlaani Ndugai kukiuka kanuni za Bunge, zikiwamo kanuni ya 5(3) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge inayoeleza kuwa, chama chenye haki kinaweza kuweka wagombea watatu katika kila kundi la wagombea wa uchaguzi wa EALA.

“Kuilazimisha Chadema kuweka wagombea zaidi ya wawili kwenye nafasi zake mbili ni kinyume cha kanuni na ndiyo maana katika kila kundi CCM nao hawakuweka wagombea watatu, badala yake wakaweka wawili,” alisema.

Aliitaja kanuni nyingine ambayo chama hicho kinadai imekiukwa ni Kanuni ya 9(1) ya Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Bunge kumruhusu mgombea wa Chama cha CUF, Thomas Malima, kujitoa ndani ya ukumbi wa Bunge akijieleza kinyume cha kanuni, kwa kuwa zinataka mgombea ajitoe kwa barua na taarifa kwa Katibu wa Bunge na nakala kwa Katibu Mkuu wa chama chake na si baada ya saa 10 siku moja baada ya uteuzi.

“Mgombea huyo hakutimiza matakwa ya kanuni hiyo na Ndugai alikaa kimya hata baada ya kukumbushwa na wabunge wa Chadema,” alisema.

Pia alisema Chadema inaitazama EALA kama sehemu inayotakiwa kupelekwa wawakilishi wenye uwezo na uzalendo kwa Taifa kwa ajili ya kusimamia na kuweka mbele maslahi ya nchi na si vyama.

“Afrika Mashariki si fursa ya ulaji, bali ni wajibu kwa Taifa letu. Tupeleke wawakilishi wenye uwezo wa kutuwakilisha,” alisema.

Pia alisema Ndugai anaposema chama hicho kinatakiwa kuzingatia mikoa, anasahau kuwa kina viti viwili tu kati ya tisa, na kwa vyovyote vile wagombea wanaweza kupatikana kutoka sehemu yoyote ndani ya nchi na si vinginevyo.

“Kama kauli hiyo ingelikuwa ni mojawapo ya kigezo, bado Chadema isingetoa watu zaidi ya mikoa miwili ambako kimetekeleza kwa kuwasilisha majina ya Wenje (Mara) na Masha (Mwanza).

“Kwa upande wa majina ya Chadema kutakiwa kuzingatia jinsia, taarifa imefafanua kuwa, chama kina haki ya kupata nafasi mbili kati ya tisa kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge,” alisema.

Katika hatua nyingine, alihoji moja ya tatu ya viti viwili ingepatikanaje ili kukidhi jinsia.

Alisema Ndugai hatoi viti vya ubunge wa EALA kama zawadi au kwa hisani yake binafsi, bali viti hivyo vinatolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Bunge kwa kuzingatia uwiano wa uwakilishi bungeni na ndiyo maana mwaka  2012, CCM ilikuwa na viti saba, lakini mwaka huu, ina viti 6.

Kuhusu chama hicho kuweka wagombea wawili na kuwa na haki ya kupata viti viwili, alisema utaratibu wa uchaguzi wa EALA unatakiwa kusimamiwa na taratibu za Bunge na ili mtu awe mbunge, ni lazima akidhi vigezo vya kuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa maana hiyo, sheria za uchaguzi wa nchi pia zinatumika, kama hivyo ndivyo, kupita bila kupingwa ni sehemu ya uchaguzi na historia inaonyesha kuwa wakati wa kuwachagua wawakilishi wa Bunge la SADC, PAP na CPA ndani ya bunge letu, kila chama kilileta viti kwa idadi kamili na wakapita bila kupingwa.

“Kitu gani kinafanya EALA iwe tofauti na kulikuwa na ajenda gani ya siri,” alihoji.

Alisema au Ndugai anataka Watanzania waanze kuulizana kati ya hao saba aliowatangaza kuwa wameshinda ni wangapi kati yao wa imani moja?

“Kama amesahau apitie upya aliowataja kuwa ndio wawakilishi wetu EALA halafu aje kutushauri kama anafanya haya kwa nia njema na si kwa lengo la propaganda na kupandikiza chuki katika Taifa ambazo CCM kimekuwa kikizitumia muda mrefu kinapoishiwa hoja zenye ushawishi na mashiko kwa umma,” alisema.

 

SAKATA LA MDEE

Wakati saa 24 za Ndugai alizompa Mdee kufika bungeni kwa hiari yake ili akahojiwe juu ya kutoa kauli za matusi dhidi yake na akishindwa kutii agizo hilo polisi wamsake na kumfunga pingu zikiisha jana, iliyokuwa ni Siku ya Kumbukumbu ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema bado wanaendelea kumsaka na hawajajua alipo.

Akizungumza jana na MTANZANIA Jumamosi kuhusu agizo la Ndugai, Mambosasa alisema Mdee bado hajapatikana na popote atakapoonekana atakamatwa.

Alisema wanaendelea kumsaka kutokana na maelekezo waliyopewa na viongozi wa juu wa jeshi hilo.

“Unaniuliza kuhusiana na huyo mbunge, vipi yupo hapo tuje tumkamate, maana tunaendelea kumtafuta kutokana na maelekezo kutoka juu,” alisema.

Pia alisema kama atapatikana, polisi haitasita kumkamata na kumpeleka anakohitajika.

“Sisi kazi yetu ni kutimiza kile tunachoelekezwa, kama atakuwa hapa sisi ndio mamlaka ya kumkamata na tutamkamata,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, alipoulizwa na MTANZANIA Jumamosi jana kama Bunge limewasiliana na Mdee na kujua atakuja lini kuhojiwa, alisema anayeweza kuzungumzia suala hilo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika.

Jana MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Mkuchika na alisema: “Yale yalikuwa ni maagizo, lakini utekelezaji wake ni hadi pale tutakapokaa na tukikutana tutawaambia.”

Mbali na Mdee, aliyedai yuko Dar es Salaam kwa ajili ya kesi ya meya wa jiji hilo na kuahidi kuitikia wito huo, juzi asubuhi wakati Ndugai akihitimisha kipindi cha maswali na majibu, pia aliagiza Mbowe kufika mbele ya kamati hiyo ili akahojiwe kwa tuhuma za kutukana mhimili huo wakati wa uchaguzi wa wabunge wa EALA.

Uamuzi huo wa Ndugai ulitokana na miongozo iliyoombwa na baadhi ya wabunge wa CCM baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika juzi.

Hatua hiyo inafika ikiwa ni takriban miezi 10 tangu Mdee alipofungiwa na kamati hiyo kuhudhuria vikao 10 vya Bunge la Bajeti lililopita.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Hombo, Fredy Azzah (Dodoma) na Harrieth Mandari

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles