Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, ametangaza kutoitetea tena nafasi hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka kumi.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana alipokutana na wanachama wa CWT katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha sherehe za kuelekea Siku ya Wanawake Dunia zinazofanyika Machi 8, kila mwaka.
“Napenda kutumia fursa hii adhimu kuwatangazia wana UWT na wanawake wengine ambao ni wana CCM, kwamba mimi Sophia Simba kwa hiari yangu mwenyewe nimeamua kutogombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT katika uchaguzi ujao,” alisema.
Sophia ambaye ni mbunge wa viti maalumu kwa miaka 22, alisema tangu alipofanikiwa kuwa Mwenyekiti wa UWT mwaka 2007, azma yake ilikuwa kuitumikia jumuiya hiyo kwa vipindi viwili tu.
“Nia yangu ni kuitumikia jumuiya hii kwa vipindi viwili tu na si zaidi ya hapo, Nitaachia kiti baadaye mwaka huu, baada ya kuitumikia jumuiya kwa mapenzi, utii, uaminifu na uadilifu mkubwa kwa kipindi cha kutosha, naona sasa ipo haja ya mimi kupumzika na kuwaachia wanawake wenzangu waendeleze pale ninapoachia, nitakabidhi kijiti hiki kwa uongozi utakaochaguliwa,” alisema.
Sophia ambaye alikuwa ni mmoja wa wanachama waliopinga kukatwa kwa jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM uliofanyika mwaka juzi, alisema hana shaka na mrithi wake kwa kuwa anaamini wapo wanawake wenye uwezo wa kuendeleza harakati hizo.
“Nimeamua niwatangazie mapema ili kuwaweka huru na kuwapa muda wa kujipanga vizuri wale wote wanaokusudia kugombea nafasi hii kubwa ndani ya jumuiya yetu, pia kutoa majibu kwa waliokuwa wakiniuliza na kunihamasisha nigombee tena,” alisema.
Pia alisisitiza kuwa anaamini wanawake waliopo pia wanaweza kuwaunganisha wanajumuiya hiyo katika kupigania haki zao za msingi, haki za ustawi wa watoto na masuala ya jamii kwa ujumla, likiwamo jukumu kubwa la kisiasa.
Sophia aliyewahi pia kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alisema kipaumbele cha UWT ni kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola.
Alisema kipindi kigumu alichokipitia katika uongozi wake, ni wakati wa mchakato wa CCM wa kumpata mgombea urais.
Katika mchakato huo, Sophia akiwa na wenzake; Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki, Adam Kimbisa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, walionyesha msimamo wao hadharani wa kutoridhishwa na hatua ya Kamati Kuu ya CCM kukata jina la Lowassa aliyetia nia ya kugombea urais.
“Katika kipindi cha mchakato wa urais, niliamini kuwa kulikuwa na mtu anafaa kuwa mgombea urais, lakini ule ulikuwa ni mtazamo wangu wa kidemokrasia, nilikuwa na kipindi kigumu,” alisema.
Licha ya kuwa na msimamo huo, lakini alibadili mawazo na kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli na kuwashawishi wanawake kumpigia kura.
Naye Katibu wa UWT Wilaya ya Temeke, Zahra Mohamed, alisema wanawake wa CCM wamesikitishwa na hatua ya Sophia kutogombea tena katika nafasi hiyo kwa kuwa alikuwa na msaada mkubwa kwao.
“Mama Sophia ametusaidia, kwa sasa kila mwanamke wa UWT anajua atumie njia gani ili apate maendeleo, kupitia semina mbalimbali alizowapa wanawake, ziliwapa mwanga na kuwafanya wajitambue katika maisha ya kila siku,” alisema Zahra.