MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA wa timu ya Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, anahofia kufukuzwa wiki hii endapo atashindwa kufanya vizuri kwenye michezo yake miwili.
Kocha huyo amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanajituma mara mbili zaidi ili waweze kuokoa kibarua chake kuanzia kwenye mchezo wa leo dhidi ya Tottenham kwenye Uwanja wa Old Trafford na ule wa Jumamosi dhidi ya wapinzani wao Manchester City kwenye Uwanja wa Etihad.
Hii ni wiki ngumu kwa kocha huyo kutokana na kikosi chake kuwa na msimu mbaya ambapo kabla ya mchezo wa leo wanashika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 18 baada ya kucheza michezo 14.
Hii ni mara ya kwanza kwa Manchester United kuwa na msimu mbaya baada ya kufanya hivyo msimu wa mwaka 1988-89, ambapo ni miaka 31 iliopita, hivyo kutokana na hali hiyo kocha huyo yupo hatarini kufukuzwa hasa akishindwa kupata matokeo mazuri wiki hii dhidi ya wapinzani hao.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu hiyo kimesema kuwa, kocha huyo amefanya mazungumzo na wachezaji wake huku akionekana kuwa na sura ya udhuni na kuwaambia kwamba, wao ndio wenye dhamana ya kumfanya kocha huyo aendelee kuwepo hapo au kuondoka kutokana na matokeo watakayoyapata wiki hii.
“Kocha ana wakati mgumu wiki hii, anakutana na Tottenham ambayo ina kocha mpya Jose Mourinho aliyekuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu baada ya kufukuzwa kazi na Manchester United, hivyo Mourinho anataka kuwaonesha kuwa yeye ni bora na walikosea kumuacha.
“Amewaambia wachezaji wake kuwa, wajitume mara mbili ya vile wanavyocheza ili waweze kuokoa kibarua chake, lakini wakishindwa kufanya hivyo basi safari yake ya kuondoka imefika kwa kuwa timu hizo mbili anazokutana nao ni washindani wake wakubwa na kila mmoja anataka kushinda,” kilisema chanzo hicho.