25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sola yaanza kukarabatiwa baada ya kusimama kwa miaka saba

*Kuanza kazi Julai 14, mwaka huu

Na Derick Milton, Simiyu

Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU), kimeanza kukarabati wa kiwanda cha kuchambua Pamba cha Sola kilichopo katika Wilaya ya Maswa, ambacho kimekaa zaidi ya miaka saba bila ya kufanya kazi.

Kiwanda hicho ambacho kilikuwa kinamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) kabla ya kufanyika kwa mgawanyiko wa mali baada ya kuundwa kwa SIMCU, hakikufanya kazi kwa muda huo baada ya umiliki wa awali kushindwa kukiendesha.

Kiwanda cha Sola ni kati ya viwanda vitatu ambavyo SIMCU imevipata kama mgao baada ya kuundwa kwake kutoka vyama vikuu vya SHIRECU na NYANZA, ambapo viwanda hivyo ni NASSA GINNERY na RUGURU GINNERY.

Wakiwa na waandishi wa habari viongozi wa SIMCU wametembelea kiwanda hicho leo Juni 23, 202 kwa ajili ya kujionea shughuli za ukarabati zinavyoendelea, ambapo wameridhishwa na kazi ya mhandisi aliyepewa kazi ya kukarabati.

Akitoa maelezo mbale ya viongozi hao, fundi kiongozi, Athuman Shabani amesema tangu wameaza zoezi la ukarabati wamefikia asilimia 20 ambapo ndani ya siku 20 zijazo zoezi zima litakuwa limekamilika.

Amesema zoezi ambalo wameanza nalo ni kufungua mashine za kuchatakata pamba na sehemu za kupitisha umeme, ambapo asilimia kubwa ya vipuli vya mashine hizo bado imara.

“Kuna vifaa vichache sana ambavyo tumekuta vimeharibika, lakini kwa kiwango kikubwa mashine bado nzima na zinafanya kazi, kwa kasi ambayo tumeanza nayo ndani ya siku 20 kiwanda kitaanza kufanya kazi,” amesema Shabani.

Mwenyekiti Kamati ya Uchumi SIMCU, Simioni Magoma, amesema katika mikakati ya Chama chao, wamepanga kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo hasa kuanza kuchakata pamba katika msimu wa mwaka huu.

Amefafanua kuwa zoezi la ukarabati linahusisha mashine za kuchambua pamba ikiwemo ukarabati wa maghala matatu ya kuanzia kwa ajili ya kutunza pamba, huku mkakati mkubwa ikiwa ni kukarabati kiwanda kizima.

“Tunashukuru sana serikali ambayo imeendelea kutuunga mkono katika zoezi hili la kuanza kufufua viwanda vyetu, tumeanza na hii sola lakini tunao mpango wa kuanza kufufua viwanda vingine ambavyo SIMCU tunamiliki,” amesema Magoma.

Kwa upande wake Meneja wa SIMCU, Shigela Magembe amesema kuwa Mhandisi Malando Zamu ndiye amepewa kazi ya ukarabati wa kiwanda hicho, kazi ambayo itatumia muda wa mwezi mmoja hadi kukamilika kwake.

Magembe ameeeleza kuwa SIMCU ilipata mkopo kutoka benki ya Kilimo (TADB) kiasi cha Sh bilioni 1.5 ambazo zinatumika kwa ajili ya ukarabati huo pamoja na kuanza ununuzi wa pamba katika msimu huu.

“Katika mkopo ambao tumepewa na TADB fedha zake ndizo zimeanza kukarabati kiwanda hiki, lakini pia kati ya fedha hizo zitatumika kuanza kununua pamba msimu huu mara baaada ya ukarabati kukamilika,” amesema Magembe.

Mwenyekiti wa SIMCU Lazaro Walwa amesema kuwa hadi kufikia Julai 14, 2022 kiwanda hicho kitakuwa kimeanza kufanya kazi ya kuchambua pamba na kuuza marobota kwani ukarabati unaoendelea utakuwa umemalizika.

Amesema kuwa mara baada ya kiwanda hicho kukamilika ukarabati wake, zaidi ya watu 300 wataajiliwa wakiwemo vibarua na kitawezesha kuinua uchumi wa wakulima wa pamba ambao watalipwa malipo ya pili mara baada ya chama hicho kuuza marobota ya pamba.

“Iwe mvua, liwe jua, mwezi Julai, 2022 lazima kiwanda kianze kufanya kazi, fedha zipo na kazi inaendelea kwa kasi, wananchi na wakulima wajiandae viwanda vyetu vinarudi kama zamani,” amesema Walwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles