24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wafugaji watakiwa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi

*Azikumbusha Halmashauri nchini ambazo hazijasajili mifugo kwa hiari

Na Samwel Mwanga, Maswa

Wafugaji mkoani Simiyu wametakiwa kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote Agosti 23, mwaka huu nakwamba kwa kufanya hivyo kutaisaidia nchi kupanga mipango ya maendeleo.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 23, 2022 wilayani Maswa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Jeremiah Wambura alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wilaya hiyo pamoja na baadhi ya wafugaji.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania,Jeremiah Wambura(Mwenye kofia )akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu(hayupo pichani)juu ya zoezi la Utambuzi wa mifugo na zoezi la Sensa ya Watu mwaka huu.(Picha Na Samwel Mwanga).

Akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Simon Berege ofisini kwake, Mwenyekiti huyo amesema lengo kubwa la kufika wilayani humo ni kuhakikisha wafugaji wanashiriki vyema kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Hivyo amewahimiza wajiandae kuhesabiwa pamoja na zoezi la utambuzi wa mifugo lakini pia kufanya usajili wa mifugo ya wafugaji.

Wambura amesema kwa wilaya ya Maswa anasikitika kuona bado haijaanza utambuzi wa mifugo licha ya zoezi hilo kutarajiwa kufikia ukingoni Agosti 31, mwaka huu kwa hiari na baada ya hapo mifugo yote ambayo haitafanyiwa utambuzi itakamatwa na kupigwa faini jambo ambalo litawaathiri wafugaji.

“Nasikitika sana kusema kuwa wilaya ya Maswa ndipo anapotoka Waziri wa Mifugo na Uvuvi, (Mashimba Ndaki) lakini Halmashauri ya wilaya ya Maswa haijaanza zoezi la utambuzi wa mifugo pia nitumie muda huu kuzisisitiza halmashauri zote nchini ambazo hazijafanya hivyo kuanza mara moja kwani ukomo wa usajili wa mifugo kwa hiari ni Agosti 31, pia sensa ni jambo la msingi kwa maendeleo ya Taifa,”amesema Wambura.

Aidha, amefafanua kuwa ameamua kufanya ziara hiyo ili kuwahamasisha wafugaji kushiriki vyema katika zoezi la Sensa itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.

“Mimi ni Mwenyekiti  wa Wafugaji Tanzania ni wajibu wangu kuwakumbusha wafugaji mambo muhimu wanayotakiwa kuyafanya kwa ajili ya maendeleo yao na mifugo yao. 

“Sio wote wenye uelewa kuhusiana na mambo haya na ndio maana nimeamua kufanya ziara kwa ajili ya kutoa elimu ili waweze kuelewa na kuwa tayari kwa ajili ya kutoa ushirikiano,” amesema Wambura.

Nae Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Haki za Wanyama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Annete Kitambi amesema ni vizuri kwa wafugaji kushiriki katika zoezi la utambuzi wa mifugo yao ili nchi iweze kujua idadi sahihi ya mifugo iliyopo na iweze kuhudumiwa kama vile ujenzi wa miundombinu ya majosho ya kuoshea mifugo sambamba na upandaji wa malisho.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simon Berege amesema wilaya hiyo ilishindwa kuanza zoezi la utambuzi wa mifugo kutokana na kukosekana kwa fedha ila watalifanya kuanzia Julai hadi Agosti, mwaka huu na kuhahidi kuwafikia wafugaji wote katika wilaya hiyo.

“Niwahakikishieni hili zoezi la utambuzi wa mifugo tutalifanya kuanzia mwezi Julai hadi Agosti mwaka huu na tutafika kila kijiji na kila mfugaji tutamfikia kabla ya tarehe ya mwisho ya zoezi hili na sasa tutaanza kutoa elimu juu ya faida ya zoezi hilo sambamba na zoezi la sensa ya watu,” amesema Berege.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles