PENDO FUNDISHA na Ramadhani Hassan – MBEYA/DODOMA
VILIO na simanzi vimetawala kwa wafanyabiashara wa soko la SIDO mkoani Mbeya, baada ya kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha hasara ya mali inayokadiriwa kufikia Sh bilioni moja.
Pamoja na hali hiyo, kumeibuka taarifa kuwa uunguaji wa masoko mkoani hapa, inawezekana unachangiwa na hujuma.
Madai ya uwapo wa hujuma katika soko hilo, yanatokana na mlolongo wa matukio ya masoko kuungua moto bila ya chanzo chake kufahamika.
Kumbukumbu zinaonyesha kabla ya tukio la juzi, soko hilo lilinusurika kuteketea kwa moto mara mbili kati ya mwaka 2011 na 2014.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio jana, baadhi ya wafanyabiashara walisema tukio hilo ni dhahiri inawezekana kuwa ni njama zenye lengo la kuwalazimisha kurudi katika soko jipya la Mwanjelwa ambalo limekosa wapangaji.
Mfanyabiashara wa duka la viungo vya vyakula, Joseph Mgogo, alisema wanaamini ni njama kwa kuwa mara ya kwanza walitakiwa kuondoka kwenda soko la Nane Nane, lakini wakamwomba Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla wajenge vibanda vya kudumu na kabla ya kujibiwa soko limeungua.
Naye Richard Jerome alisema wanasikitika kuona tukio hilo limetokea wakati hawajapata jibu la msingi kutoka serikalini.
“Tulimwomba mkuu wa mkoa tujenge vibanda vya matofali hatujajibiwa, leo (juzi) soko limeteketea na kuunguza kila kitu, huwezi kuona hizi ni hujuma za wazi?” alihoji.
Mfanyabiashara mwingine, Suzi Kibona, alisema soko hilo halina miundombinu ya umeme wala hakuna watu wanaopika chakula ndani, jambo ambalo linakuwa gumu kutokea itilafu ya moto.
“Ni vigumu kutokea moto, haiwezekani kwa akili ya kawaida, moto umesababishwa uwake wakati hakuna mama lishe, miundombinu ya umeme wala vibanda vya mafundi wa kushona nguo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya soko hilo, Mikaeli Amon, alisema yeye na kamati yake walifanya ukaguzi kabla ya kukabidhi soko kwa walinzi, huku kila kitu kikiwa salama.
Alisema hadi dakika za mwisho wanaondoka eneo la tukio, hakukuwa na mtu aliyebaki ndani ya soko na kuwaacha walinzi wa Kampuni ya New Imara wakiendelea na kazi yao.
Amon alisema alishangaa usiku kupata taarifa za kuungua kwa soko hilo.
“Tunashindwa tusemeje, hatujawahi kupewa majibu ya uchunguzi uliofanyika katika matukio ya moto yaliyotokea kipindi cha nyuma, leo tena tunarudishwa nyuma na moto, hapa wataalamu watusaidie hali hii hadi lini?” alihoji Amon.
Katibu wa soko hilo, Alhanusi Ngogo, alisema ukosefu wa miundombinu ya maji na umakini mdogo wa watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ndiyo sababu kubwa ya kuteketea kwa soko hilo ambalo lilikuwa ni chanzo cha mapato kwa wafanyabiashara zaidi ya 3,000.
Alisema hasara wanayokadiria kutokana na moto huo ni zaidi ya shilingi bilioni moja, na changamoto kubwa kwa wafanyabiashara hao ni fedha za mikopo waliyokopa katika taasisi mbalimbali za fedha.
“Serikali inatakiwa kuangalia njia itakayoweza kusaidia kutatua matatizo ya moto kwa kuwa mara kwa mara magari ya kikosi cha zimamoto yamekuwa yakikabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji na hivyo mali kuteketea, wakati uwezekano wa kuziokoa ni mkubwa,” alisema.
Kuhusu uokoaji wa mali, alisema suala hilo lilikumbana na vikwazo kutoka kwa polisi waliokuwa wanarusha mabomu ya machozi, kitendo kilichowafanya wafanyabiashara kuingiwa hofu na kushindwa kusogea karibu kuokoa mali zao.
MBUNGE SUGU
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, aliwataka wafanyabiashara wa soko hilo wawe watulivu na kwamba kuungua kwa soko hilo kusihusishwe na mambo mengine.
“Baadhi ya wafanyabiashara wanahusisha na hujuma za kutaka kuwalazimisha kuhamia soko jipya… hili ni tukio la kawaida kama yanavyotokea matukio mengine,” alisema.
Hata hivyo, alisema tatizo la maji ni kubwa jijini hapo na kusisitiza ipo haja ya Serikali kutengeneza vituo vya maji vitakavyosaidia pindi linapotokea tatizo.
Alisema bila kufanya hivyo moto utaendelea kusababisha hasara kubwa kwa wananchi.
KAULI YA MCHUNGAJI
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbeya Mjini, Aman Mwaijande, alisema kuna haja ya viongozi wa dini na Serikali kukaa na kutafakari jinamizi la matukio hayo.
“Hali iliyopo sasa inatisha, wanaoumia ni wananchi wanaorudi nyuma kwa maendeleo… wakati wa kumrudia mwenyezi Mungu atusaidie na kutuonyesha njia ya kukabiliana na hali hii,” alisema.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, aliwataka wananchi kuwa watulivu na watoe ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na kuongozwa na Mkuu Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika kuchunguza chanzo cha moto huo.
MATUKIO YA NYUMA
Matukio ya kuungua moto kwa masoko jijini hapa, yameendelea kuzua maswali mengi.
mwaka mwaka 2006, liliungua Soko Kuu la Mwanjelwa na wafanyabiashara walihamishiwa soko la Sido, lakini nalo likaungua 2011.
Soko hilo la Sido liliungua tena mwaka 2014 na sasa limeungua na kuteketea kabisa.
Pia soko la Uhindini liliungua lote mwaka 2009 na chanzo cha moto hadi sasa hakijafahamika.
Licha ya kuwapo madai ya hujuma za masoko hayo kuchomwa moto kwa makusudi, lakini hakuna mamlaka iliyothibitisha hujuma hizo.
WAZIRI MWIGULU
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kufanya uchunguzi wa kina utakaobaini chanzo cha moto ulioteketeza soko hilo.
Mwigulu aliyasema hayo akiwa mjini Dodoma jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema jeshi hilo linatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kutoka na majibu ambayo yatakuwa suluhisho la matukio ya aina hiyo.
“Kipindi cha nyuma palikuwapo matukio ya moto maeneo mbalimbali na yalikomeshwa, kama mlivyosikia, Mbeya tena moto umetokea na kuteketeza soko,” alisema Mwigulu.
Kutokana na hali hiyo, aliziagiza halmashauri zote kuchukua tahadhari za moto ili kuweza kuona namna ambavyo wanaweza kukomesha matukio kama hayo.
Alisema kama miundombinu ingekuwa mizuri, moto ulioteketeza soko hilo, ungedhibitiwa mapema kabla haujawa mkubwa.