NA HADIA KHAMIS-DAR ES SALAAM
SODA, chumvi na soda vinaongoza kwa kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo shinikizo la damu, MTANZANIA limeelezwa.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania unaonyesha asilimia 27 ya Watanzania wamebainika kuwa na shinikizo la damu.
Akizungumza na Jukwaa la Waandishi wa Habari na Wahariri wa Kupambana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza Tanzania (TJNCDF), Profesa Andrea Swai alisema magonjwa yasiyoambukiza ndiyo yanayoongoza kwa idadi kubwa ya vifo.
Alisema asilimia tisa ya Watanzania wote wamebainika kuwa na ugonjwa wa kisukari huku ugonjwa wa saratani ukiongoza mara mbili ya wagonjwa wanaopokelewa hospitalini.
“Magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ndiyo yanaongoza kwa vifo na hii inatokna na vyakula tunavyokula ikiwa ni pamoja na chumvi, soda na chips,” alisema Profesa Swai.
Alisema ili kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni lazima waandishi wa habari kutumia kalamu zao vema ili kuweza kuhabarisha umma.
Alisema kila mmoja anajukumu la kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuzingatia anafanya mazoezi ya kutosha ili kuimarisha afya ya mwili wake.
“Ifike wakati tuwe na utamaduni wa kufanya mazoezi kwa ajili ya viungo vyetu hii itatusaidia kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Profesa Swai.