27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Snura, Chura wake wafungiwa

SNURAANA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesitisha wimbo na video ya ‘Chura’ wa msanii, Snura Mushi ‘Snura Majanga’, kuchezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hadi itakapofanyiwa marekebisho.

Wimbo na video hiyo umetokana na maudhui ya utengenezwaji wake ambayo hayaendani na maadili ya Mtanzania.

Pia Serikali imesitisha maonyesho yote ya hadhara ya msanii huyo, mpaka atakapokamilisha taratibu za usajili wa kazi zake za sanaa katika Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Licha ya hivyo, Serikali imewataka wasanii wajiulize kabla ya kubuni kazi zao za sanaa kwa kufikiria wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao namna watakavyozipokea.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Zawadi Msalla, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wasanii wanapotunga nyimbo zao wavae nafasi za wanaowadhalilisha na waelewe kwamba sanaa si uwanja wa kudhalilisha watu.

“Serikali imechukizwa na kazi hiyo ya Snura kwa kuwa si tu inadhalilisha tasnia ya muziki, bali inadhalilisha utu wa mwanamke kiasi kwamba jamii inaanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya sanaa kwa ujumla,” alieleza Msalla.

Msalla aliongeza kwa kuwataka wananchi kutojiingiza katika makosa ya sheria ya mtandao, kwa kusambaza wimbo huo kwa njia yoyote ya kimtandao.

Pia alivitaka vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi za sanaa, kabla ya kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za sanaa.

Hata hivyo, inadaiwa baada ya Snura kuitwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa ajili ya utetezi wake alishindwa kujieleza alipotakiwa kueleza anajisikiaje kumdhalilisha mwanamke wakati yeye ni mwanamke.

Inadaiwa Snura alikosa la kujibu zaidi ya kuomba msamaha kwa Serikali imsamehe kwa alichokifanya.

Snura alipotakiwa na Mtanzania kuelezea alivyopokea kifungo hicho, alidai kwamba atazungumza na waandishi wa habari leo katika mkutano wake.

“Leo (jana) sizungumzi chochote na waandishi nitazungumza kesho (leo) katika mkutano wangu pale Idara ya Habari Maelezo nitatoa yangu,” alieleza Snura.

Kabla wimbo huo haujatoka, Snura alikuwa akipiga picha za vipande vikimuonyesha akiwa maeneo mbalimbali akitikisa umbo lake akimuwakilisha chura.

Baadhi ya vipande hivyo alivionyesha kama chura akiwa anafua, anapika, anaumwa ametundikiwa dripu na nyinginezo jambo ambalo lilizua maswali mengi ya kuhusu maadili ya Mtanzania kwa mashabiki wake na wadau wa muziki kwa ujumla.

Wimbo wa video hiyo inakuwa ya pili kwa msanii huyo kufungiwa kutokana na maadili mabovu, ambapo awali video ya Snura ‘Majanga’ ulifungiwa na kutolewa katika kinyang’anyiro cha vipengele vya kugombea tuzo za muziki za Kili huku mwenyewe akilalamika kutotendewa haki.

Pamoja na wimbo huo, wimbo mwingine uliotolewa katika mchakato huo na kufungiwa pamoja na ‘Majanga’ ni video ya wimbo wa ‘Uzuri wako’ ya msanii, Juma Jux.

Nyimbo nyingine zilizowahi kufungiwa kutokana na kukiuka maadili ya Mtanzania ni ‘Zigo’ wa Ambwene Yessaya ‘AY’ aliomshirikisha Diamond Platinumz wa ‘Zigo’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles