29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta azidi kuinanga rasimu ya Jaji Warioba

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

MAREGESI PAUL NA RACHEL MRISHO, DODOMA

MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ameendelea kusisitiza kuwa rasimu ya Katiba mpya iliyosimamiwa na Jaji Joseph Warioba imejaa kasoro.

Kutokana na hali hiyo, amesema Bunge Maalumu la Katiba limelazimika kuiboresha kwa kuwa kila kitu kinachoandikwa na binadamu hakiwezi kuwa sahihi.

Sitta alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akipokea ujumbe wa viongozi wa vyama na asasi za watu wenye walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

“Kuna mambo yanaendelea hapa, wengine wanayakejeli, ingawa ni ya kawaida kuelekea kupata Katiba mpya.

“Jambo lolote lililoandikwa na binadamu haliwezi kuwa sahihi, hii rasimu siyo msahafu kiasi kwamba haiwezi kubadilishwa, hiyo siyo sahihi kabisa.

“Hao wanaosema tunafanya mambo ya tume, waendelee kusema tu, lakini Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya kurekebisha upungufu hata msemeje, rasimu hii tumegundua ina upungufu kadha wa kadha, lazima tuiboreshe.

“Bahati nzuri hata waandishi wengine mko hapa, yaani hata nyinyi mmeamua kujiingiza katika jambo hili hadi mnaandika ‘ma-editorial’.

“Kuna vita kubwa na nzito, kuna watu wanapiga vita taasisi hii, mimi siwajali, yaani sijawahi kuona watu wakikosa uzalendo kiasi hiki, lakini sisi tutaendelea hata mkifanyaje,” alisisitiza Sitta.

Pamoja na hayo, Sitta alizungumzia mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba na kusema linaendeshwa vizuri na kwamba Katiba mpya itakayopatikana itakuwa nzuri na wananchi wataifurahia.

“Kwa maana hiyo, ndugu zangu walemavu msiwe na wasiwasi, haya mnayoyasema hapa nitahakikisha yanaingizwa kwenye majumuisho, kwani hata leo mchana (jana) nitakutana na Kamati ya Uongozi ambayo nitaieleza juu ya haya mapendekezo yenu,” alisema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ushauri cha Watu Wenye Ulemavu, Kaganzi Rutachwamagyo, aliwasilisha ripoti ya mapendekezo wanayotaka yawemo katika Rasimu ya Katiba mpya.

Katika mapendekezo hayo aliyosema yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Felician Mkude, Rutachwamagyo alisema yamefanyika kwa sababu rasimu ya Katiba imezungumzia walemavu bila kuwaangalia kwa undani.

“Kuna msemo katika Biblia sijui uko sura gani na katika kitabu kipi, lakini unaeleza kwamba Yesu anasema hakuja kutengua Torati bali kuitimiliza.

“Kwa mfano, kifungu cha 113 cha Rasimu ya Katiba kinasema Rais atachagua watu wenye ulemavu watano kuwa wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini sisi tunaona hii siyo sawa kwetu,” alisema.

Mjadala wa jumla ndani ya Bunge Maalumu la Katiba unaanza leo kwa Kamati 12 za Bunge hilo kuwasilisha taarifa zao.

Mjadala huo unaanza wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wanaounda kundi la Ukawa wakiwa bado wamegoma kurudi, huku hofu kubwa ikitawala kama wajumbe waliobaki wataweza kupitisha Ibara za rasimu hiyo kwa kupata idadi ya theluthi mbili kwa kila upande wa Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ndo kawaida ya dolla inayotaka kuanguka, huwa inatengeneza maadui wengi kwa ubabe. Mbio za sakafuni huishia ukingoni, ngoja tuone mfalme sitta na vibaraka wengine waendelee na ujuaji na ubabe tuone mwisho wa siku wataipeleka wapi nchi. Langu jicho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles