MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amekiongoza kikosi chake kwenda Kanda ya Ziwa ambako kitacheza michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United, akiahidi kuvuna pointi zote sita.
Wachezaji 22 wa timu hiyo waliondoka jijini Dar es Salaam jana kwenda Bukoba, ambapo kesho wataumana na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba kabla ya Septemba 29 kupepetana na Biashara United, Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Msimu uliopita, Kagera Sugar iliinyanyasa Simba kwa kuitandika kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu.
Kagera iilaza Simba mabao 2-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Kaitaba kabla ya kuichapa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Aussems ana kibarua kingine kizito cha kuvuna pointi tatu dhidi ya Biashara United inayonolewa na Amri Said ambaye alikuwa kocha wa kwanza msimu uliopita kuiliza Simba wakati huo akiifundisha Mbao FC iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kagera inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa ilizovuna katika michezo yake mitatu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Aussems alisema wamejipanga vilivyo kuhakisha wanapata ushindi dhidi ya Kagera na kufuta uteja wao.
“Tumejipanga kulipa kisasi, hatukupata matokeo mazuri msimu uliopita lakini safari hii tunataka kuondoka na pointi tatu.
“Tunajua haitakuwa rahisi kutokana na ubora wa kikosi cha wapinzani wetu ambao hawajapoteza mchezo.
“Maandalizi tuliyofanya si kwa mechi ya Kagera pekee, tunajua tuna michezo miwili huko hivyo tumemaliza kila kitu hapa, tutaanza na Bukoba na kumalizia kazi kwa Biashara,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.
Simba itaendelea kumkosa nahodha wake, John Bocco ambaye anaeuguza majeraha ya goti, lakini mshambuliaji Mbrazil, Wilker Henrique Da Silva yupo fiti.
Da Silva anaweza kucheza michezo hiyo baada ya kupona jeraha la goti.