Azam yapania kushangaza Zimbabwe

0
735

Mohamed Kassara -Dar es salaam

BAADA ya kutua salama jijini Harare nchini Zimbabwe, Kocha Mkuu wa Azam FC, Etiene Ndayiragije bila kupoteza muda ameanza kuwapa mbinu wachezaji wake zitakazowawezesha kupindua meza ugenini kwa kuichapa Triangle United, katika mchezo utakaopigwa Jumamosi hii Uwanja wa Gibbo.

Azam ina kibarua kizito cha kusaka ushindi  dhidi ya Wazimbabwe ugenini, katika mchezo huo wa marudiano wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.

Wana lamba lamba hao waliishangazwa nyumbani kwa kucharazwa bao 1-0, katika mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 15, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Azam inahitaji kupambana kufa au kupona kushinda mchezo huo ili kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika.

Kikosi cha Azam kiliondoka kwa makundi mawili, la kwanza lililongozwa na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Idd Nassoro ‘Cheche’ lilitua Harare Jumapili iliyopita, kabla kundi la pili liliwa na Ndayiragije kuwasili nchini humo juzi.

Ndayiragije ambaye ni Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, alitua na wachezaji watano walikuwa kwenye kikosi hicho kilichoivaa Sudan na kuchapwa bao 1-0, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) uliochezwa Jumapili  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu kutoka Harare jana, Afisa Habari wa Azam , Jaffar Idd alisema wanaendelea kujifua vikali kwa lengo la kuhakikisha wanalipa kisasi na kusonga mbele.

“Tayari wachezaji wetu watano waliokuwa Stars wameungana na wenzao na kufanya mazoezi jana jioni, kocha ameanza kupanga mikakati ya mwisho ya kuhakikisha timu inapata ushindi ugenini na kutinga hatua ya makundi.

Kupoteza mchezo wa kwanza hakujatuvunja moyo, tunaendelea kujipanga kwa lengo la kupindua matokeo, kikubwa Watanzania watuombea ili tuweze kufanikiwa katika mapambano yetu,”  alisema Idd.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here