29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yatakata Moro

SIMBA NA POLISI2TIMU ya soka ya Simba, jana ilizinduka na kuwapa raha mashabiki wake baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba kupanda kutoka nafasi ya tisa hadi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 20, kutokana na mechi 14.
Azam ndio waliopo kileleni na pointi 25 baada ya kushuka dimbani mara 13, sawa na Yanga, lakini ‘Wanalambalamba’ hao wapo kileleni kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa upande wao, Polisi wamebaki na pointi 19 wakiwa nafasi ya tano.
Kwa upande mwingine, ushindi wa jana ni wa tatu kwa Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic, tangu aanze kukinoa kikosi hicho katika mechi za Ligi Kuu baada ya awali kuzifunga Ndanda FC ya Mtwara na JKT Ruvu ya Pwani.
Katika mchezo huo wa jana, Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kwa Ibrahimu Ajibu aliyeunganisha vema krosi iliyochongwa na beki Mganda, Jjuuko Murushid.
Mshambuliaji Elias Maguli aliipatia Simba bao la pili dakika ya 63 baada ya kipa Tony Kavishe kulazimika kutoka golini kufuatia makosa yaliyofanywa na Mohamed Mpopo katika harakati za kuokoa hatari hiyo.
Simba ndio waliouanza mchezo wa jana kwa kasi ambapo baada ya kupata bao la kwanza, walizidisha mashambulizi langoni mwa Polisi na kupata kona dakika ya 20 na dakika mbili baadaye ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi aliikosesha Simba bao dakika ya 25, baada ya krosi aliyopiga kutambaa mwamba wa juu mwa lango la Polisi.
Dakika 26 na 41, Simba walipata kona nyingine baada ya kufanya mashambulizi langoni mwa wapinzani wao lakini walishindwa kuzitumia nafasi hizo kutokana na Polisi kulinda vema lango lao.
Polisi ambao walitumia muda mwingi kuusoma mchezo wa Simba, walikosa bao la wazi dakika ya 43 baada ya Imani Mapunda kushindwa kutumia vema pasi ya Anafi Selemani.
Mshambuliaji Said Bahanuzi aliyejiunga na Polisi akitokea Yanga, alikosa bao dakika ya 44 baada ya shuti lake kutoka nje kidogo ya lango la Simba.
Kipindi cha kwanza, mwamuzi Paul David kutoka Mtwara aliwaonya kwa kadi ya njano Seleman Kassim wa Polisi aliyerusha mpira vibaya na Ibrahim Ajibu wa Simba kwa kumchezea madhambi, James Ambrose.
Polisi walianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanya shambulizi kali lililotoka nje kidogo ya lango ambapo dakika za 61 na 62 walifanikiwa kupata kona ambazo hata hivyo hazikuwa na madhara wa Simba.
Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa kipa Ivo Mapunda aliyepata maumivu makali wakati akidaka mpira na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Manyika dakika ya 58 ya mchezo.
Polisi walifanya mabadiliko ya kuwatoa Lulanga Mapunda na James Ambrose na nafasi zao kuchukuliwa na Said Mkangu na Nicholas Kabipe, huku Simba ikiwatoa Ramadhan Singano ‘Messi’ na Hassan Ramadhan ‘Kessy’ na kuwaingiza Awadh Juma na Nassor Masoud ‘Chollo’.
Dakika ya 74 Ajibu almanusura aipatie Simba bao la tatu baada ya kushindwa kuunganisha pasi ya Okwi na dakika ya 81 Bahanuzi alikosa bao la wazi baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa wapinzani wao.
Simba: Ivo Mapunda/Manyika Peter, Hassan Ramadhan ‘Kessy’/Nassor Masoud ‘Chollo’, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Jjuuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano “Messi’/Awadh Juma, Abdi Banda, Alias Maguli, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Okwi.
Polisi: Tony Kavishe, Mohamed Mpopo, Hassan Mganga, Laban Kambole, Anafi Selemani, Lulanga Mapunda/Said Mkangu, Seleman Kassim, James Ambrose/Nicholas Kabipe, Said Bahanuzi, Imani Mapunda na Edward Christopher.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles